Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb)
ameelekeza Jeshi la Uhifadhi (JU) na Jeshi la Polisi (PT) kuendelea
kushirikiana katika utatuzi wa changamoto zinazoikabili Sekta ya Maliasili na
Utalii ikiwemo matukio ya ujangili na utoroshaji wa nyara za Serikali.
Ameyasema hayo leo Agosti 9, 2025 alipokuwa akifungua rasmi kikao kazi
kilichoandaliwa na Wizara ya Maliasili
na Utalii kati ya Jeshi la Uhifadhi na Jeshi la Polisi kilichofanyika katika
Hifadhi ya Ziwa Manyara, Mkoani Arusha.
“Pamoja na mafanikio hayo na ushirikiano uliopo baina ya majeshi yetu,
zipo changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza na kuhitaji ushirikiano
zaidi wa pamoja katika kuzitatua ikiwa ni pamoja na zile zinazowakumba maafisa
na askari wetu pindi wanapotekeleza majukumu yao ya kupambana na majangili wa
aina mbalimbali wa nyamapori, meno ya tembo, samaki na ulishaji wa mifugo ndani
ya hifadhi,” amesisitiza Mhe. Chana.
Aidha, Mhe. Chana ametaja matukio hususan ya mifugo kuingizwa katika maeneo ya hifadhi, ambapo mara kadhaa
askari hao wamekuwa wakivamiwa na makundi ya wafugaji kuanzia watu 50 na
kuendelea wakiwa na silaha za jadi kwa lengo la kushinikiza kurudishiwa mifugo
yao.
Awali akimkaribisha Waziri Dkt. Chana, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili
na Utalii anaeshughulikia Uhifadhi Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba
ameahidi kusimamia utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa hususan uwepo wa
vikao vya mashirikiano na Jeshi la Polisi katika ngazi mbalimbali ikiwemo
Kanda.
Naye Kamishna wa Polisi Charles Mkumbo, kwa niaba ya Jeshi la Polisi
ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jitihada kubwa inazofanya katika
kuimarisha mashirikiano, na kuahidi kuwa Jeshi hilo litaeendelea kushirikiana
na Jeshi la Uhifadhi kikamilifu, katika ulinzi wa Maliasili kwa maslahi mapana
ya taifa.
Pamoja na Makamanda wengine, kikao hicho kinashirikisha, Viongozi
waandamizi Wizara ya Maliasili na Utalii, Makamishana wa Polisi watano,
Makamanda wa Polisi wa Mkoa 17, wakuu wa
taasisi za Jeshi la Uhifadhi pamoja na Mkamanda waandamizi wa
Jeshi la Uhifadhi.
0 Maoni