Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza ratiba ya kuchukua fomu
za uteuzi kwa wagombea wa vyama 14 vya siasa waliopendekezwa kugombea nafasi za
Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo
inaanza kesho tarehe 09 Agosti, 2025.
Mkurugenzi wa INEC, Ndugu, Kailima Ramadhani akizungumza jijini Dodoma
leo tarehe 08 Agosti, 2025 amewataja wagombea watakaochukua fomu kesho tarehe
09 Agosti, 2025 kuwa ni kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), National
Reconstruction Alliance (NRA) na Alliance for African Farmers Party (AAFP).
“Hadi leo tarehe 08 Agosti, 2025, tumepokea barua kutoka katika vyama vya
siasa kumi na nne (14) zikiainisha tarehe na muda ambao wanachama wa vyama vyao
waliowapendekeza kugombea nafasi za Kiti cha Rais na Makamu wa Rais watafika
ofisi za Tume zilizopo Njedengwa Jijini Dodoma kwa ajili ya kuchukua Fomu za
Uteuzi,” amesema Ndugu. Kailima.
Amevitaja vyama vingine na tarehe za wagombea kuchukua fomu kuwa ni
pamoja na na Chama cha MAKINI tarehe 10 Agosti, 2025, The National League for
Democracy (NLD) tarehe 10 Agosti, 2025, United Peoples’ Democratic Party (UPDP)
tarehe 10 Agosti, 2025 na African Democratic Alliance Party (ADA – TADEA)
tarehe 11 Agosti, 2025.
Vyama vingine ni Union for Multiparty Democracy (UMD) tarehe 11 Agosti,
2025, Tanzania Labour Party (TLP) tarehe 11 Agosti, 2025, Chama Cha Kijamii
(CCK), tarehe 12 Agosti, 2025, Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), tarehe 12
Agosti, 2025, Alliance for Democratic Change (ADC), tarehe 12 Agosti, 2025,
Democratic Party (DP) tarehe 13 Agosti, 2025 na National Convention for
Construction and Reform (NCCR – MAGEUZI) tarehe 15 Agosti, 2025.
Ndugu Kailima amesema tayari Tume imeviandikia vyama hivyo vya siasa
barua kuvijulisha kuhusu ratiba hiyo ya utoaji fomu za uteuzi.
“Aidha, ni muhimu tukumbuke kuwa, ratiba hii inahusu vyama kumi na nne
(14) pekee vilivyowasilisha taarifa hadi kufikia leo tarehe 08 Agosti, 2025,
hivyo iwapo vyama vingine vitajitokeza, tutaandaa ratiba husika na
kuwajulisha,” amesema.
Amevipongeza vyama vyote vya siasa kwa kuendelea kufanya maandalizi ya
Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 na kuongeza kuwa, Tume kwa upande wake itazingatia
katiba, sheria na kanuni wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
0 Maoni