Timu ya Tanzania ya wanawake kutoka kituo cha Future Stars
Academy cha jijini Arusha, imefanikiwa kuchukua nafasi ya pili katika michuano
ya vijana wanaotoka kwenye mazingira magumu (Homeless World Cup) yaliyofanyika
kuanzia tarehe 22-30 Agosti 2025, jijini Oslo, Norway, yakishirikisha timu 60
kutoka mataifa 48.
Timu ya Future Stars Academy imefanikiwa kuchukua nafasi
hiyo baada ya kushinda mchezo wa fainali ya daraja la pili la michuano hiyo
dhidi ya Austria kwa mabao 5 kwa 4. Mabao ya Tanzania yalifungwa na Loyce
Dismas, Susan Michael, Varian Issa na Sarah Jacob.
Mshindi wa kwanza wa jumla kwa timu za wanawake ilikuwa
Uganda baada ya kushinda mchezo wa fainali ya daraja la kwanza dhidi ya
Romania. Kenya ilifanikiwa kushika nafasi ya tatu baada ya kushinda fainali
dhidi ya Mexico kwenye daraja la tatu la michuano hiyo.
Kwa upande wa timu za wanaume Misri ilichukua ubingwa wa
jumla huku Ureno ikishinda kwenye daraja la pili na Poland kwenye daraja la
tatu. Tanzania haikuwakilishwa na timu ya wanaume.
Michuano hiyo ya timu za wachezaji wanne-wanne huanza kwa
raundi ya kwanza katika makundi ambapo washindi wa kwanza huingia raundi ya
pili ya makundi katika daraja la kwanza; washindi wa pili huingia kwenye
makundi ya daraja la pili na washindi wa tatu kwenye makundi ya daraja la tatu.
Katika raundi ya pili timu huchuana tena hadi kufikia
fainali ya kila daraja ambapo mshindi wa daraja la kwanza hutangazwa bingwa wa jumla;
mshindi wa daraja la pili huwa mshindi wa pili wa jumla na mshindi wa daraja la
tatu huwa mshindi wa tatu wa jumla. Tanzania imeshinda kwenye fainali ya daraja
la pili.
Mashindano haya huandaliwa kila mwaka na taasisi ya Homeless
World Cup yenye makao yake makuu nchini Uholanzi ikishirikiana na shirika la
Salvation Army.
Balozi wa Tanzania anayewakilisha katika nchi za Nordic,
Baltic na Ukraine, Mobhare Matinyi, aliwapongeza vijana hao kwa ushindi
walioupata na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa
walikuja wanne tu bila mchezaji wa akiba hata mmoja.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu timu ya Tanzania kushiriki
mashindano haya ambayo mwakani yatafanyikia nchini Mexico.
Na. Ubalozi wa Tanzania, Stockholm, Agosti 31, 2025.
0 Maoni