Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Mhe. Doto Mashaka Biteko amezindua Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Ajenda
ya Wanawake, Amani na Usalama 2025-2029.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa
Mpango huo Agosti 19, 2025 uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya
Ulinzi wa Amani (TPTC) kilichopo Kunduchi mkoani Dar es Salaam, Dkt. Biteko
amezitaka Wizara na Taasisi za Serikali na Wadau mbalimbali wa maendeleo
kuhakikisha wanatenga Bajeti ya utekelezaji wa Mpango huo ili kutimiza malengo
yake.
"Naomba nitoe rai kwa Wizara zote
zenye dhamana ya agenda hii; Tanzania Bara na Zanzibar; mkasimamie na kutekeleza
mpango huu kama ilivyokusudiwa ili kufikia malengo stahiki," amesema Dkt.
Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amesema katika
utekelezaji wa Mpango huo amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wakiwa Wenyeviti
wa Kamati za Ulinzi na Usalama kwenye maeneo yao kusimamia kikamilifu
utekelezaji wa Mpango huo kwa kushirikiana na wadau waliopo.
"Niwaombe kuhakikisha kuwa mnatoa
elimu na kuhamasisha, ushiriki wa wanawake na wanaume katika hatua zote za
kuzuia, kutatua migogoro na ujenzi wa amani, ulinzi na usalama," amesisitiza
Dkt. Biteko.
Akitoa salamu za Wizara Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy
Gwajima amesema katika kuandaa Mpango huo, uainishaji wa maeneo mahsusi ya
vipaumbele vya Mpango umezingatia maudhui ya Azimio Na. 1325 la Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ameongeza kuwa Mpango huo unabainisha
maeneo manne (4) ya kipaumbele na kuwasilisha masuala ya msisitizo katika
utekelezaji ikiwemo eneo la kuzuia linalosisitiza umuhimu wa kujumuisha
mitazamo ya kijinsia katika mikakati ya kuzuia migogoro na mbinu za tahadhari
za mapema, eneo la ushiriki linalosisitiza haja ya ushiriki wa wanawake katika
kufanya maamuzi katika ngazi zote katika michakato ya amani, utatuzi wa
migogoro na kujenga amani.
Akiyataja maeneo mengine kuwa ni eneo
la ulinzi linalotoa wito wa kuimarishwa kwa hatua za kuwalinda wanawake na
wasichana dhidi ya unyanyasaji wa kingono na kijinsia wakati na baada ya
migogoro na eneo la Msaada na Urejeshaji wa Hali linalohimiza utekelezaji wa
mbinu au jitihada zinazozingatia usawa wa kijinsia katika juhudi za usaidizi na
uokoaji na wakati wa urejeshaji wa hali ya ustawi na utulivu baada ya migogoro.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi huo
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Stergomena Tax amesema Tanzania
imetambua kuwa ili kuimarisha amani Wanawake lazima washirikishwe katika Ajenda
hii hivyo uwepo wa Mpango huo utaweka mikakati mahususi ya kushirikisha
wanawake katika amani na usalama na kuimarisha juhudi za Kitaifa katika kuzuia
migogoro kukuza amani jumuishi na kulinda Haki za Wanawake na wasichana.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe amesema Ajenda Wanawake Amani
na Usalama ni muhimu kwa maendeleo ya wanawake na Watanzania wote hivyo katika
kutekeleza Ajenda hii Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mikakati na
mipango mbalimbali katika kuhakikisha Wanawake. wanashirikishwa katika masuala
ya amani na usalama na kukuza Usawa wa Kijinsia na Ustawi wa Wanawake.
Naye Mkurugenzi wa Kanda wa UN Women Anna
Mutabati amesema katika utekelezaji wa Mpango huo Tanzania haianzi mwanzo bali
inaendeleza mipango na mikakati iliyopo inayotekelezwa kuhusu masuala ya
Wanawake Amani na Usalama chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo utaleta mabadiliko zaidi katika
nyanja mbalimbali.
0 Maoni