Wananchi wa kijiji cha Buturu Wilayani
Butiama Mkoani Mara wameipongeza Serikali kwa kuwajengea daraja ambalo linakuwa
mkombozi kwa kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kijifungua pamoja na
watoto kusombwa na maji wakati wa kwenda shule kutokana na kuwepo na bonde
katika barabara kuu ya kijiji hicho.
Bw. Maningu kasombi, Mwenyekiti wa
kijiji cha Buturu anasema kabla ya ujenzi wa daraja hilo la mawe wakazi wa
kijiji hicho walikuwa inawalazimu kutumia gharama kubwa katika usafiri kwa
kuzunguka vijiji vingine ili kufikia
huduma za kijamii na ameweka wazi kuwa wajawazito asilimia kubwa walikuwa
wanajifungulia njiani au majumbani kwa kukosa miundombinu mizuri ya barabara.
" Ubovu wa barabara ulikuwa
unafanya akinamama kujifungulia njiani na wakati mwingine usafiri unakosekana
hivyo wengi walikuwa wanajifungulia nyumbani lakini kwa sasa tunatumia barabara
hii muda wowote na usafiri umekuwa wa gharama nafuu ukitofautisha na mwanzo
ambapo tulikuwa tunatumia mpaka elfu 15 kufika butiama,” amesema Maningu.
Licha ya changamoto hiyo ya wanawake
kijifungua njiani pia Kijiji hicho kilikuwa chini kiuchumi kutokana na
kushindwa kuuza mazao yao kwa wakati na kupelekea kudorora kwa mazao lakini kwa
sasa wanaipongeza Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo limeleta faraja
kijini hapo na kuinua uchumi wa wananchi.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Buturu Bi. Grace
Richard anaipongeza Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo limeenda kuongeza
maudhurio ya wanafunzi shuleni hapo tofauti na awali ambapo ilikuwa inawalazimu
Wazazi na Waalimu kuwavusha watoto katika bonde hilo ili waweze kwenda shule
kutokana na bonde hilo kuwa na maji mengi hali ambayo ilikuwa ikichangia utoro
shuleni.
"Ilikuwa ikifika kipindi cha
masika shule yetu ilikuwa na changamoto ya utoro kutokana na watoto wengi
kushindwa kuvuka kwenye bonde na kuja shule ukizingatia wanafunzi wengi wapo
upande wa pili na ilikuwa inatulazimu waalimu na wazazi kuwavusha watoto ili
waweze kufika shule hii ilikuwa inaathiri wakati mwingine ufundishaji."
Awali akisoma Taarifa ya mradi wa
ujenzi wa Daraja la mawe Meneja wa
Tarura Wilaya ya Butiama Mhandisi Rashidi Kavandama amesema mradi huo
umegaharimu kiasi cha Shilingi Milioni
299.26 na daraja lina ulefu wa Mita 32 na upana wa Mita 7.7 ambapo daraja hili
ni sehemu ya Miradi ya maendeleo inayojengwa na Serikali ya awamu ya sita kupitia fedha za mfuko wa bodi ya Barabara.
Mhandisi Kavandama ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo umekamilika kwa 100% na
kukamilika kwa mradi huo kumesaidia wananchi kuzifikia huduma za kijamii kwa
urahisi kama huduma za kiuchumi na
kijamii kama vile Afya, Elimu na Biashara.
Aidha, Kiongozi wa mbio za Mwenge
Kitaifa Ndugu Ismail Ali Ussi amezindua daraja hilo ambalo limekuwa kiungo
muhimu kwa wakazi wa kijiji cha Buturu na Chifu Wanzangi na kusema daraja hilo
limeleta matumaini kwa Wananchi wa eneo hilo.
" Ombi langu kwa wananchi wa eneo
hili nitumie fursa hii kuwaasa mtunze miundombinu hii ya daraja ili iweze kuwa imara zaidi na kutumika kwa
muda mrefu zaidi."
Ussi pia ameipongeza Tarura kwa
kutumia mawe kujenga daraja hilo kwani kumeweza kupunguza gharama za ujenzi kwa
kiasi kikubwa tofauti kama wangeamua kulijenga kwa kutumia zege.
" Nawapongeza ofisi ya Tarura
Mkoa wa Mara na Wilaya ya Butiama kwa kuwa wazalendo kwelikweli wameamua
kujenga Daraja hili kwa kutumia mawe na limegharimu Fedha isiyozidi milioni 500
hili ni jambo la kuwapongeza kweli kwa uzalendo wao."
0 Maoni