Ili kuendana na Dira ya Taifa 2050,
Serikali ya awamu sita imedhamiria kuijenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) ili kuwezesha huduma zote kutolewa ndani ya jengo moja ambapo hospitali
hiyo itakuwa ni mifumo ya kisasa ili kuendena na mapinduzi ya teknolojia ya
tiba duniani.
Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi
Mtendaji wa MNH Dkt. Delilah Kimambo wakati wa mahojiano na shirika la
Utangazaji Tanzania (TBC) juu uwekezaji wa miundombinu na vifaa tiba Hospitali
ya Taifa Muhimbili wakati wa serikali ya awamu ya sita na kueleza kuwa mradi
ambao utagharimu USD .468 Mil (takriban TZS. 1.23 Trilioni) ambapo kati ya
fedha hizo USD.364 Mil zitatoka Korea Kusini.
“Tutakwenda kuweka jiwe la msingi la
tatu. Itajengwa hospitali kubwa tena ya kisasa kabisa hapa Muhimbili Upanga na
itaongeza huduma kwa kiwango kikubwa sana. Kwa mfano, kwa huduma ya mama mtoto
pekee tutakuwa na vitanda zaidi ya 350, na vitanda vyote hivyo siyo kwamba ni
kwa ajili ya huduma zile za kawaida, hapana, sisi tutakuwa tunatoa zile za
kibobezi. Kwa hiyo utaona uwezekaji huo ulivyo na manufaa makubwa” amesema Dkt.
Kimambo.
Kwa upande mwingine, Dkt. Kimambo
ameeleza kuwa licha ya juhudi kubwa za uwekezaji ambazo zimeelekezwa katika ujenzi
wa majengo mapya, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, pamoja na kuboresha mifumo
ya usimamizi wa huduma katika hospitali, bado kuna hatua zaidi zinazochukuliwa
ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Aidha ameainisha kuwa Muhimbili mpya
inatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kulaza wagonjwa, ambapo idadi
ya vitanda itaongezeka kutoka 1,500 vya sasa hadi kufikia 1,775 huku teknolojia
ya kisasa kama akili unde ikitarajiwa kurahisisha utoaji wa huduma.
0 Maoni