Wadau mbalimbali wameaswa kuunganisha
nguvu na kushirikiana katika kuhakikisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa
wa Kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 2025-2029 inafikia malengo
yaliyokusudiwa ili kuondoa vikwazo vyote vinavyowazuia wanawake kushiriki
kikamilifu katika masuala ya amani na usalama.
Hayo yamesemwa mkoani Dar es Salaam
Agosti 18, 2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake
na Makundi Maalum Dkt. John Jingu wakati wa akifungua Kongamano kuelekea
Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na
Usalama 2025-2029.
Dkt. Jingu amesema ni muhimu
kuimarisha elimu na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia kama
msingi wa amani endelevu, sambamba na kuweka mifumo thabiti ya ufuatiliaji na
tathmini ili kuhakikisha kuwa hatua zinazochukuliwa zinafanikiwa na zinaendana
na malengo ya Mpango Kazi huo.
"Kwa kufuata mwelekeo huu,
Tanzania itaendelea kujenga hadhi yake kama mfano wa kuigwa, ikithibitisha kuwa
ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama si ndoto bali ni hatua halisi za
maendeleo, usawa na ustawi wa kijamii." amesema Dkt. Jingu.
Kwa upande wake Naibu Mwakilishi
Mkaazi wa UN Women Katherine Gifford, amesema Mpango Kazi wa Kitaifa wa
Kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 2025-2029 ni mwelekeo mzuri
katika kuhakikisha Mwanamke anashirikishwa katika masuala ya amani na usalama
hivyo Mpango huo unapaswa kuwekwa katika utekelezaji zaidi ili kutimiza malengo
yaliyokusudiwa.
Aidha, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya
Ulinzi wa Amani Brigedia Jenerali George Itang'are ameishukuru Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuandaa Mpango Kazi
huo ambao ni mwanzo wa mabadiliko makubwa ya kuhakikisha Mwanamke
anashirikishwa katika masuala muhimu ya amani na usalama.
Na. WMJJWM - Dar es Salaam
0 Maoni