WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Belarus, Alexander Turchin na kujadiliana naye masuala ya uwekezaji,
biashara, nishati, madini, elimu, afya, teknolojia na kilimo kwenye kikao
kilichofanyika jana (Jumanne, Julai 22, 2025) ofisini kwa mwenyeji wake, mtaa
wa Sovetskaya, jijini Minsk.
Katika mazungumzo hayo,
Waziri Mkuu Majaliwa alimweleza mwenyeji wake kuwa, mbali na kuimarisha
mahusiano ya kidiplomasia anataraji kuwa ziara hiyo itaongeza chachu ya nchi
hiyo kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji,
elimu, afya na upatikanaji wa zana za kisasa kwenye kilimo kutokana na fursa
mbalimbali zilizoko nchini.
Alisema mazungumzo yao
yamefungua milango ya kuimarisha uwekezaji, fursa za biashara na masomo katika
vyuo vya elimu ya juu, na kwamba wamekubaliana na mwenyeji wake kuwa Mawaziri
wake na Naibu Makatibu Wakuu walioko kwenye ziara hiyo wakutane ili kuanza
majadiliano rasmi ya kufanikisha nia ya kampuni ya Minsk Tractor Plant OJSC ya
kuleta kiwanda kama hicho nchini.
Aliwaeleza baadhi ya
wajumbe wa kikao hicho wanaotoka Chama cha Wafanyabiashara cha Belarus kwamba
hivi sasa Tanzania imepunguza muda wa kupata leseni, imeongeza maeneo ya
uwekezaji (TISEZA) na imeboresha sheria za kikodi ili kuhamasisha uwekezaji
nchini.
Aliwaeleza fursa nyingine
za kuwekeza Tanzania ni uwepo wake kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya
ya kikanda ya SADC na Eneo Huru la Biashara barani Afrika (ACfTA) pamoja na
uwepo wa nchi sita zinazoizunguka Tanzania na hazina bandari (land-locked
countries) ambazo zina wakazi wengi.
Katika kikao hicho,
Mawaziri Wakuu wote wawili walishuhudia utiaji saini wa hati tatu za
makubaliano na maktaba mmoja baina ya mawaziri wa nchi hizo mbili. Hati hizo
zilizosainiwa leo zinahusu mashauriano ya kisiasa; makubaliano ya kuendeleza
sekta ya kilimo na sekta ya elimu.
Aidha, mkataba
uliosainiwa leo ni baina ya Chama cha Wafabiashara, Viwanda na Kilimo ya
Tanzania (TCCIA) na Chama cha Wafabiashara wa Belarus unaolenga kukuza
ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Waziri
Mkuu wa Belarus, Alexander Turchin alimshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kufanya
ziara ya Kiserikali nchini humo na kuipa heshima nchi hiyo kupokea kiongozi
mkuu kutoka Tanzania kwa mara ya kwanza.
Alisema Belarus inaiona
Tanzania kuwa mdau muhimu wa ushurikiano katika nyanja mbalimbali na hasa
ikizingatiwa kwamba nchi hiyo inao utaalamu (expertise) katika nyanja nyingi
ambazo zimegusiwa wakati wa majadiliano yao. “Tuko tayari kutoa ushirikiano
kwenye maeneo uliyoyataja na wala sioni haya kusema hivyo kwa sababu nchi yetu
inao utaalamu mkubwa kwenye maeneo uliyoyaainisha,” alisema.
Alisema mazungumzo yaliyofanyika leo baina ya viongozi hao wakuu ni mwanzo wa ushirikiano wa kudumu ambao utasaidia kukamilisha masuala yaliyoibuliwa kutokana na ziara hiyo. “Ziara hii ni fupi na hatuwezi kukamilisha kila jambo, lakini maeneo yote ya usalama wa chakula, utoaji wa huduma za tiba, kilimo na elimu yanaweza kukamilishwa na timu zetu,” alisema.
Alitumia fursa hiyo
kumtakia heri Mheshimiwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye
uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Mapema asubuhi, Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea kiwanda cha kutengeneza dawa cha Republican
Unitary Production Enterprise “Belmedpreparaty” na kiwanda cha kutengeneza matrekta
na zana za kilimo cha Minsk Tractor Plant OJSC.
Katika ziara hiyo,
Mheshimiwa Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi,
Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Bw. Shariff Ali Sharriff, Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, Naibu Katibu
Mkuu Wizaya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu pamoja Naibu Katibu Mkuu Kilimo, Dkt.
Stephen Nindi.




0 Maoni