Wadau wa biashara ya
mazao ya misitu wameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kupitia
Shamba la Miti Sao Hill, kwa juhudi zake za kutatua changamoto zinazowakabili
kwa wakati, hatua iliyowezesha kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara
hiyo.
Pongezi hizo zilitolewa
wakati wa kikao kati ya viongozi wa Umoja wa Wadau wa Uvunaji wa Mazao ya
Misitu (UWASA) na uongozi wa TFS – Shamba la Miti Sao Hill, kilichofanyika leo
katika ukumbi wa makao makuu ya shamba hilo mkoani Iringa.
Akizungumza kwenye kikao
hicho, Mwenyekiti wa UWASA, Bw. Chesco Ng’umbi, alisema licha ya kuwepo kwa
changamoto kadhaa katika mnyororo wa uvunaji na usafirishaji wa mazao ya
misitu, TFS imeendelea kuonyesha ushirikiano na kujibu changamoto hizo kwa
wakati.
“Sisi kama wadau wa
uvunaji katika Shamba la Sao Hill tunaishukuru TFS kwa kuwa sikivu na
kushughulikia changamoto zetu kwa wakati. Ushirikiano huu umechochea maendeleo
na kutuwezesha kufanya shughuli zetu kwa ufanisi,” alisema Bw. Ng’umbi.
Aidha, alisisitiza
umuhimu wa elimu ya mara kwa mara kwa wadau kuhusu taratibu za kisheria katika
biashara ya mazao ya misitu ili kuhakikisha shughuli hizo zinaendeshwa kwa
mujibu wa sheria na kuepuka migongano isiyo ya lazima.
“Tunaomba TFS iendelee
kutupatia elimu kuhusu biashara ya mazao ya misitu, hasa kuhusu taratibu na
sheria. Vikao vya aina hii viendelezwe kwa ajili ya kujengeana uelewa wa
pamoja,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mhifadhi
Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoram, aliwataka wadau wa misitu
kuhakikisha wanalipa vibali kwa wakati na kufuata utaratibu wa uvunaji na
usafirishaji wa mazao hayo ili kuepuka migongano na taasisi za udhibiti.
“Mwaka wa fedha 2025/2026
umeanza. Tunawasihi waliopata migao ya uvunaji kuhakikisha wanakamilisha
taratibu za ulipaji na uvunaji kwa wakati. Hii itachangia kuongeza mapato ya
serikali kupitia TFS,” alisema Yoram.
Aliongeza kuwa mifumo
inayotumika katika TFS inaunganishwa na taasisi nyingine, hivyo ni muhimu kwa
wadau kuhakikisha nyaraka zao zinakuwa sahihi na halali wakati wote wa
utekelezaji wa shughuli zao shambani.
“Tukumbuke kauli ya
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mifumo inatakiwa kusomana. Hivyo,
taarifa zisizolingana kati ya taasisi huleta mkanganyiko. Tuongeze uaminifu na
usahihi wa nyaraka,” alieleza Yoram.
Aidha, alisisitiza
matumizi ya teknolojia ya kisasa katika biashara ya mazao ya misitu ili
kuongeza tija, kurahisisha taratibu, na kuhakikisha wadau wanapata faida
stahiki kupitia mfumo rasmi wa kibiashara.




0 Maoni