Kamati ya Ukaguzi ya
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ikiongozwa na Mwenyekiti wake
CPA Ally Rashid imeanza ziara ya kukagua Miradi ya ujenzi wa Miundombinu ya
barabara mkoani Singida.
Kamati hiyo Mkoani
Singida imetembelea miradi miwili ya ujenzi wa daraja la mawe Mkonjigwe lenye
urefu wa mita 42 linalojengwa katika barabara ya
Chibumagwa-Sasajila-Makasuku-Itetema Kata ya Sasajila Wilayani Manyoni pamoja
na ujenzi wa barabara ya Mandewa 69 yenye urefu wa Km. 0.89 kwa kiwango cha lami inayojengwa katika Manispaa ya Singida.
Akielezea hali ya
utekelezaji wa miradi hiyo Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Ibrahim
Kibasa amesema kuwa mradi wa daraja la
mawe umetekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilihusisha uchimbaji
wa msingi wa daraja, ujenzi wa msingi wa daraja yaani 'Raft Foundation' na
nguzo za daraja.
Awamu ya pili
ilihusisha ujenzi wa ukuta nusu
duara, mabawa ya daraja, kingo kwenye
maingilio ya daraja na eneo la kutokea, ujenzi wa kuta za mawe kwaajili ya
kuunganisha nusu duara, kujaza kifusi, kupanga mawe, kumwaga jamvi eneo la juu
la daraja na kuchonga barabara za maingilio ya daraja.
Akielezea umuhimu wa
daraja hilo kiuchumi na kijamii Mhandisi Kibasa amesema kuwa kukamilika kwa
ujenzi wa daraja hilo kutasaidia kukuza uchumi wa wananchi kwa kurahisisha
usafiri na usafirishaji wa samaki, chumvi na nafaka ndani ya Wilaya ya Manyoni
na kupunguza vifo vya wananchi vinavyotokana na maji wakati wa kuvuka mto
hususani majira ya mvua.
Kwa upande wa hali
utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Mandewa 69 Mhandisi Kibasa ameeleza kuwa
mpaka sasa Mkandarasi anametekeleza kazi Kwa asilimia 88 na kwa sasa anaendelea
na kazi ya ujenzi wa vivuko vya magari na watembea kwa miguu na mradi huo
unatarajia kukamilika tarehe 31/7/2025.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya TARURA CPA Ally Rashid amesema kuwa wao
wameona utekelezaji wa kazi hizo na ndio lengo la ziara yao na kuishauri TARURA
Mkoa wa Singida kuendelea kusimamia Miradi hiyo ili iweze kutekelezwa kwa
kuzingatia ubora sambamba na kuwashirikisha wananchi katika ulinzi wa
miundombinu hiyo.



0 Maoni