Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa
Ridhiwani Kikwete ameipongeza Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kukuza
ujasiriamali na kuongeza elimu ya fedha kwa wananchi wengi zaidi kupitia
Programu ya Imbeju
Waziri Kikwete ametoa
pongezi hizo kwenye uzinduzi wa shirika lisilo la kiserikali linalohamasisha
ujasiriamali miongoni mwa vijana la National Enterprise Development Chamber
(NEDC) uliofanyika mwishoni mwa wiki.
“Taasisi ya CRDB Bank
Foudation mnafanya kazi kubwa sana katika kuwainua vijana kupitia Programu yenu
ya Imbeju. Mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha mnayoitoa. Kujitoa kwenu
kuilea NEDC nalo ni jambo muhimu litakalosaidia kuwajumuisha vijana wengi
kwenye huduma rasmi za fedha,” amesema Waziri Kikwete.
CRDB Bank Foundation
imedhamini uzinduzi wa NEDC inayoziunganisha biashara changa hasa za kibunifu
ambazo nyingi zinamilikiwa na vijana,
kuwaunganisha wafanyabiashara, wawekezaji pamoja na taasisi za umma ili
kujenga ushirikiano utakaoboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini,
malengo ambayo ni miongoni mwa vipaumbele tunavyotekeleza CRDB Bank Foundation.
Mkurugenzi Mtendaji wa
CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema wanashirikiana na kila mdau
kuboresha maisha ya watu kutoka jamii zilizotengwa kifedha na kiuchumi kwa
kutoa mafunzo ya ujasiriamali, elimu ya fedha na kuwapa mitaji wezeshi
wajasiriamali wanaokidhi vigezo.
“Katika kuhamasisha
maendeleo ya ujasiriamali na ubunifu, tunachochea ukuaji wa ubunifu na biashara
changa za vijana, tunawawezesha vijana na wanawake kupitia mafunzo ya stadi za
elimu ya fedha, ujasiriamali, usimamizi wa biashara, utunzaji wa kumbukumbu na
mbinu za upatikanaji wa rasilimali fedha pamoja na Kuchochea ubunifu kupitia
programu za kukuza na kuendeleza biashara changa,” amesema Tully.
Ili kuwa na maisha bora,
Tully amesema ni muhimu kwa wananchi hasa wa kipato cha chini kujengewa wa
kifedha , kukuza utamaduni wa kuweka akiba na uwekezaji pamoja na kuwajumuisha
katika huduma rasmi za fedha vijana na wanawake bila masharti magumu.
“CRDB Bank Foundation
(CBF) inatambua nguvu ya ushirikiano wa kimkakati katika kuleta mabadiliko
chanya kwani ndio njia ya uhakika ya kufungua fursa zaidi kwa vijana na
wanawake wajasiriamali nchini. Tunashirikiana na serikali kuendeleza
ujumuishaji wa kifedha na kukuza suluhisho bunifu na tunashirikiana na sekta
binafsi kuongeza uwekezaji katika ujasiriamali na elimu ya fedha,” amesema
Tully.
Mwanzilishi na Mkurugenzi
Mtendaji tena National Enterprise Development Chamber (NEDC), Jesse Madauda
amesema wataendelea kushirikiana na serikali, taasisi za umma na binafsi pamoja
na wabia wengine wanaopenda kumwinua Mtanzania kiuchumi.
“Kwa kuunganisha nguvu,
rasilimali na mikakati, tunaamini tunaweza kuharakisha ukuaji wa biashara
changa zenye uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika jamii,” amesema Madauda.
0 Maoni