Ofisi ya Msajili wa
Hazina (OMH) imejiwekea lengo la kukusanya kiasi cha Sh2 trilioni kama mapato
yasiyo yakikodi katika mwaka wa fedha 2025/26, imebainishwa.
Hayo yalisemwa mapema
wiki hii na Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu wakati wa ufunguzi wa
mafunzo elekezi ya siku nne kwa wakuu wa taasisi za umma yaliyoandaliwa na OMH
kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi.
Kiasi kinachotarajiwa
kukusanywa ni zaidi ya lengo la Sh1.6 trilioni ambalo serikali iliiwekea Ofisi
ya Msajili wa Hazina kukusanya mwaka huu wa fedha.
“Ili tuweze kufikia lengo
letu la kukusanya Sh2 trilioni itatubidi tuongeze bidii kwa asilimia 100 ya
tulivyokuwa tunafanya mwaka wa fedha uliopita,” alisema Bw. Mchechu.
Katika mwaka wa fedha
uliopita (2024/25) Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikusanya kiasi cha Sh1.028
trilioni kama mapato yasiyo yakikodi.
Miongoni mwa vyanzo vikuu
vya mapato yasiyo yakikodi ni Gawio---Mapato haya yanatokana na Mashirika na
Taasisi zinazofanya biashara na yanakusanywa kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni
SURA 212 (Kifungu cha 180) na Sheria ya Mashirika ya Umma Sura 257 (Kifungu cha
15(2)(b)).
Vyanzo vingine
ni michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi--- Kifungu cha 12 (3) cha Sheria ya
Fedha za Umma Sura 348 kinazitaka taasisi za umma (zisizo kwenye kundi la
gawio) kuwasilisha asilimia kumi na tano ya mapato ghafi kwenda Mfuko Mkuu wa
Serikali.
Pia kuna mapato
mengineyo ambayo huhusisha asilimia 70 ya mapato ya ziada ya taasisi za umma,
marejesho ya mikopo na riba na mawasilisho yatokanayo na mtambo wa kuhakiki na
kuwezesha mawasiliano (TTMS) kati ya Tanzania na nchi nyingine.
Msajili wa Hazina
anaamini kuwa mafunzo elekezi kwa Kundi hili la pili linalojumuisha watendaji
wakuu 114 wakiwemo walioteuliwa hivi karibuni pamoja na walioko katika nafasi
zao kwa muda mrefu lakini hawakubahatika kupatiwa mafunzo, yatakuwa chichu ya
mageuzi katika mashirika ya umma.
Na. Mwandishi wa OMH
0 Maoni