Serikali kupitia Wizara
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imepokea kwa
masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watoto watano waliopoteza maisha katika
ajali ya moto iliyotokea usiku wa Julai 28, 2025 katika Makao ya Watoto ya
Igambilo, Manispaa ya Tabora.
Katika taarifa
iliyotolewa jana na Waziri wa wizara hiyo, Dkt. Dorothy Gwajima, Serikali
imetoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huo
mzito, huku ikitoa wito kwa jamii kuwaombea waliopoteza wapendwa wao faraja,
subira na nguvu katika kipindi hiki kigumu.
"Tunasikitika kwa
msiba huu mkubwa uliogharimu maisha ya watoto wetu. Tunaungana na familia zao
na wote walioguswa katika maombi na pole nyingi," amesema Dkt. Gwajima.
Waziri huyo pia
ameliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha ajali
hiyo ya moto, na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha, Dkt. Gwajima
ametoa wito kwa wamiliki na wasimamizi wa Makao yote ya Watoto nchini kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara wa mifumo ya umeme, sambamba na kuweka miundombinu ya
kudhibiti majanga ya moto ili kuzuia ajali za aina hiyo kujirudia.
Serikali imesema tayari
imechukua hatua kuhakikisha majeruhi wa tukio hilo wanapata matibabu bure, huku
watoto wengine waliokuwepo katika makao hayo wakihamishwa na kupelekwa katika
mazingira salama, sambamba na kusaidiwa kisaikolojia na kijamii kupitia Maafisa
Ustawi wa Jamii.
"Wizara itaendelea
kufuatilia kwa karibu mwenendo wa tukio hili na kuchukua hatua stahiki za
kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto wote walioko katika Makao ya Watoto
nchini," imeeleza taarifa hiyo.
Tukio hilo linaibua
maswali juu ya hali ya usalama katika baadhi ya vituo vya kulelea watoto
nchini, huku wadau wa haki za watoto wakitaka hatua madhubuti zichukuliwe
kuzuia madhara kama haya siku za usoni.
0 Maoni