Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi imewataka watendaji wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutoa taarifa
mapema kwa vyama vya siasa kuhusu utaratibu wa kuwaapisha mawakala.
Hayo yamesemwa mkoani
Shinyanga leo Julai 21, 2025 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,
Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele wakati akifungua mafunzo kwa
watendaji wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba mwaka huu kwa
tarehe itakayotangazwa na Tume.
“Wakati wa kuapisha
mawakala, toeni taarifa mapema kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria, kanuni
na maelekezo ya Tume na kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia
kura ili kuviwezesha kupanga mawakala,” amesema Jaji Mwambegele.
Amewasisitiza watendaji
hao kuhakikisha vifaa vya uchaguzi wanavyopokea kutoka Tume, wanavihakiki,
kuvikagua na kuhakikisha vinasambazwa kwenye vituo vyote na kila mkuu wa kituo
anapata vifaa vyote vya uchaguzi vinavyohitajika mapema.
Amewataka kuhakikisha
kuwa siku ya uchaguzi wanaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia
kura kufunguliwa saa 1:00 kamili asubuhi na kufanya mawasiliano na Tume pale
ambapo ushauri utahitajika kuhusiana na masuala ya uchaguzi.
Akifungua mafunzo kama
hayo Kisiwani Pemba, Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk amewaasa
watendaji hao kufanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na
maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume.
“Jitahidini na mjiepushe kuwa vyanzo vya
malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi. Hakikisheni
mnazingatia ipasavyo Katiba, Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali
yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume,” amesema Jaji Mwambegele.
Amewataka kuwashirikisha
wadau wa uchaguzi kwenye maeneo wanayopaswa kushirikishwa kwa mujibu wa Katiba,
Sheria, Kanuni, miongozo na maelekezo ya Tume.
Amewakumbusha kuhusu
wajibu wao wa kuhakikisha wanavitambua vituo vya kupigia kura mapema ili
kubaini mahitaji maalum ya vituo husika na kuhakikisha kunakuwa na mpangilio
mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
“Ajira za watendaji wa
vituo zizingatie kuajiri watendaji wenye weledi, wanaojitambua, wazalendo,
waadilifu na wachapakazi na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao
hawana sifa za kufanya shughuli za uchaguzi,” amesema Jaji Mbarouk.
Mafunzo hayo yanafanyika
kwa siku tatu kwenye mikoa mbalimbali nchini kwa siku tatu na yanawajumuisha
waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa
uchaguzi ngazi ya jimbo.
Tume imeyagawa mafunzo
hayo kwenye awamu mbili ambapo awamu hii ya pili inahusisha mikoa ya Simiyu,
Shinyanga, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Mwanza, Mara, Dar es Salaam, Pwani,
Rukwa, Katavi, Manyara, Arusha, Songwe na Mbeya.
Awamu ya kwanza
ilifanyika tarehe 15 hadi 17 na ilihusisha watendaji kutoka mikoa ya Morogoro,
Singida, Dodoma, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Mjini Magharibi, Geita, Kagera,
Mtwara, Lindi, Tabora, Kigoma, Tanga, Kilimanjaro, Ruvuma, Iringa na Njombe.
0 Maoni