Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa asilimia 80 ya vifo nchini vinaweza kuzuilika endapo Watanzania wataamua kubadili mtindo wa maisha ikiwemo kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi ya mara kwa mara.
Amesema hayo tarehe 27
Julai, 2025 jijini Dodoma wakati akimwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim
Majaliwa katika kilele cha msimu wa Sita wa NBC Dodoma Marathon 2025 ambayo
imelenga kukusanya fedha kwa ajili ya kuokoa afya ya mama na mtoto.
“Taarifa ya Shirika la
Afya Duniani ya mwaka 2022, inaeleza kuwa, mazoezi ya mara kwa mara kama vile
kukimbia, yana uwezo wa kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo kwa zaidi ya
asilimia 35.Vile vile, mazoezi ya mwili husaidia kujikinga na magonjwa mengine
yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, saratani na magonjwa
mengine mengi,” ameeleza Dkt. Biteko.
Kwa upande wa Tanzania,
Dkt. Biteko amesema kuwa asilimia 33 ya Watanzania watu wazima wana uzito
uliopitiliza na asilimia 28 wana shinikizo la damu ambapo ameeleza kuwa
magonjwa hayo yanachangia zaidi ya asilimia 40 ya vifo vya mapema lakini asilimia
80 ya vifo hivyo vinaweza kuzuilika kwa kubadili mtindo wa maisha.
Dkt. Biteko ameipongeza
Benki ya NBC kupitia NBC Dodoma Marathon kwa kuunga mkono Serikali katika
nyanja mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya kwani katika mwaka 2025 Marathon hiyo
imelenga kuendeleza mapambano dhidi ya Saratani ya shingo ya kizazi kwa
kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya
Ocean Road.
Pia, imelenga kutoa
ufadhili wa masomo ya Wakunga kupitia Taasisi ya Benjamin Mkapa ili kusaidia
kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi na kutoa ufadhili kwa mafunzo
ya Wauguzi Maalum wa kusaidia watoto
wenye changamoto ya usonji (Autism), kwa kushirikiana na AMREF Afrika.
Vilevile, Dkt. Biteko amesema kuwa tangu NBC
Dodoma Marathon kuanzishwa mwaka 2020 imekuwa ni moja ya vilelezo vya kujenga mshikamano, uzalendo wa kweli na
kutatua matatizo mbalimbali katika jamii ikiwemo changamoto za kiafya.
Dkt. Biteko ameipongeza
NBC Dodoma Marathon kwa kuendelea kuimarika kwani mwaka 2024 ilihusisha
washiriki 8,000 na mwaka huu imekuwa na
washiriki zaidi ya 12,000 sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 50.
Vile vile, mwaka 2024 NBC
Dodoma Marathon ilikusanya kiasi cha Shilingi Milioni 300 huku mwaka 2025
ikikusanya kiasi cha Shilingi Milioni 700 sawa na ongezeko la mapato ya zaidi
ya asilimia 133.33.
Amesema kuwa, Serikali
itaendelea kushirikiana na wadau kama NBC ambao wameendelea kutumia mashindano
ya mbio kuimarisha afya za wananchi na kuchangia masuala mbalimbali ya kijamii
ikiwemo kuokoa afya za watu.
Katika hatua nyingine,
Dkt. Biteko ametoa rai kwa Wizara ya Afya, Serikali za Mitaa, Mashirika ya
kiraia, Sekta binafsi na wananchi wote
kufanya mbio na mazoezi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku ili kuweza
kujikinga na matatizo ya afya ambayo wananchi wanaweza kuyapata.
“Nitashukuru sana kusikia
kila Taasisi imetenga kwa uchache siku moja kwa mwezi ili kuwa na mazoezi ya
pamoja, hii itasaidia kuimarisha afya zetu na kujenga Taifa Imara,” amesisitiza
Dkt.Biteko
Vilevile ameipongeza Wizara ya Afya, kwa Kampeni ya MTU NI AFYA ambayo
inawahamasisha Watanzania kufanya mazoezi kwa angalau dakika 30 kila siku, kula
lishe bora, kupima afya mara kwa mara na kujiepusha na tabia hatarishi.
Kwa upande wake, Mhe.
Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
amesema mbio za NBC Dodoma Marathon zimekuwa kivutio kwa wanamichezo wengi
kushiriki kutokana na kundaliwa vizuri ambapo amesema kuwa Wizara hiyo
itaendelea kuiunga mkono benki ya NBC katika maandalizi ya mbio hizo ambazo
zimekuwa na matokeo chanya.
Amesema Wizara ya
Utamaduni, Sanaa na Michezo itaendelea kuweka mazingira mazuri ya wananchi
kushiriki michezo mbalimbali pamoja na kuendelea kujenga viwanja vya michezo
katika maeneo mbalimbali ikiwemo Arusha, Dodoma na Dar es Salama ili kuwezesha
vijana kujiimarisha kimichezo na kiafya.
Awali, Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi alisema NBC Marathon imekuwa ni moja ya
alama za sekta binafsi katika kuwekeza kwenye sekta ya afya na nyinginezo, akieleza kuwa katika kipindi
cha miaka mitano mbio hizo zimefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 1,
ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika Sekta ya Afya.
Ametaja mafanikio ya
marathon hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu na kufanikisha kupimwa Saratani ya
shingo ya kizazi kwa Wanawake zaidi ya 200,000 na kufadhili matibabu kwa
wagonjwa 4,800 waliogunduliwa na kansa hiyo katika Hospitali ya Ocean Road.
Amesema, NBC Dodoma
Marathon imetoa ufadhili kwa Wakunga 100 katika chuo cha Wakunga Morogoro kwa
ushirikiano na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation huku lengo likiwa ni kufadhili wakunga 500 ifikapo
2028.
Pia ameeleza kuwa, NBC
Dodoma Marathon imechangia ujenzi wa Wodi maalum ya Wanawake katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili na maeneo mengine katika maendeleo ya sekta ya afya.
Amesema msimu wa sita wa
NBC Dodoma Marathon umehusisha wakimbiaji 12,000 na wamefanikiwa kukusanya
shilingi milioni 700 kwa ajili ya afya ya mama na mtoto ikilenga kuwapatia uchunguzi wa mwanzo wa saratani ya
kansa ya kizazi wanawake 10,000, kutoa ufadhili kwa wakunga 100 na kuanzisha
mpango mpya wa masomo kwa wauguzi 100 watakaoshughulika na watoto wenye
changamoto ya usonji.
NBC Dodoma Marathon 2025
iliyokuwa na kaulimbiu ya Kata Wese Okoa Maisha imehusisha wanariadha kutoka
ndani na nje ya nchi ambapo washindi wamepewa zawadi za jumla ya shilingi
milioni 80. Aidha imekabidhi pikipiki 10 kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni