Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
(INEC) imewahakikishia viongozi wa vyama vya siasa kuwa kutakuwa na uwanja sawa
kwa vyama vyote wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuhakikisha
kila chama kinafanya mikutano yake kwa mujibu wa ratiba.
Mwenyekiti wa Tume Huru
ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele ameyasema hayo leo
tarehe 27 Julai, 2025 wakati akifungua mkutano wa Tume na Viongozi wa Vyama vya
Siasa jijini Dodoma.
”Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi, inawahakikishia kuwepo kwa uwanja sawa kwa vyama vyote wakati wa
kampeni kwa kuhakikisha kila chama kitafanya mikutano yake kwa mujibu wa ratiba
itakayokuwa imepitishwa na kamati ya ratiba ngazi ya Taifa inayoratibu ratiba
ya kampeni ya wagombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais, kamati ya jimbo
inayoratibu ratiba ya wagombea wa ubunge na kamati ya kata inayoratibu ratiba
ya wagombe wa udiwani,” amesema Jaji Mwambegele.
Amewasisitiza viongozi
hao wa vyama vya siasa kuwasihi wagombea na wafuasi wao kufanya kampeni za
kistaarabu na kuepuka kufanya vitendo vitakavyoweza kusababisha uvunjifu wa
amani na utulivu wa nchi.
”Kipindi cha kampeni
kunakuwa na joto kali la kisiasa linalotokana na baadhi ya watu kukosa
uvumilivu wa kisiasa hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi,”
amesema.
Jaji Mwambegele
amewahakikishia viongozi hao wa vyama kuwa katika kipindi cha utoaji fomu za
wagombea ambacho kinaanza tarehe 09 Agosti, 2025 hadi tarehe 27 Agosti, 2025
kwa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais na tarehe 14 Agosti, 2025 hadi
tarehe 27 Agosti, 2025 kwa wagombea wa Ubunge na Udiwani, Tume itazingatia
sheria.
” Tume inapenda
kuwahakikishia kwamba, katika kipindi cha utoaji wa fomu za uteuzi na siku ya
uteuzi wa wagombea, tutasimamia Katiba, Sheria na Kanuni ili kuhakikisha kila
mwenye sifa ya kugombea anapata haki ya kupewa fomu na kuteuliwa pale
atakapotimiza masharti ya uteuzi,” amesema.
0 Maoni