Tanzania, Morocco, Ethiopia waendeleza ubabe katika utalii Afrika

 

Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism) kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025 imeonesha Tanzania ikiendelea kung’ara katika sekta ya utalii, kwa kuongoza Afrika kwa mapato na kuingia kwenye tatu bora ya nchi zenye ongezeko kubwa la watalii barani.

Ripoti hiyo, iliyotolewa mwishoni mwa Mei, imefanya tathmini ya mwenendo wa utalii duniani kwa kulinganisha takwimu za mwaka huu na zile za mwaka 2019, kabla ya janga la UVIKO-19 – ikiwa ni kipimo cha kuonesha urejeo wa hali ya kawaida na mafanikio ya nchi mbalimbali katika sekta hiyo muhimu kiuchumi.

Tanzania Yatinga Tatu Bora Afrika kwa Ongezeko la Watalii

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania imepanda hadi nafasi ya tatu Afrika kwa ongezeko la idadi ya watalii, ikiwa imeongezeka kwa asilimia 50 ikitanguliwa na Morocco (60%) na Ethiopia (52%). Ongezeko hilo limeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 20 bora duniani katika kipengele hicho, ikiungana na mataifa kama Brazil, Albania, Qatar na Saudi Arabia.

Yashika Namba Moja Afrika kwa Ongezeko la Mapato

Katika upande wa mapato yatokanayo na utalii, Tanzania imeibuka kidedea barani Afrika kwa kuongoza kwa ongezeko la asilimia 66 ikilinganishwa na mwaka 2019. Imeizidi Tunisia (62%) na Morocco (49%), na kushika nafasi ya 12 duniani, ikiweka jina lake sambamba na mataifa tajiri kama Norway, Moldova, Brazil, Qatar na Saudi Arabia.

Dkt. Abbasi: Mbegu za Mikakati Zimezaa Matunda

Akizungumzia mafanikio hayo akiwa Paris, Ufaransa, Katibu Mkuu wa Utalii na Mwenyekiti wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi alisema, “Haya ni matokeo ya mikakati thabiti. Hatukuweza kuyapata haya kwa kukaa ofisini na kusubiri miujiza.”

Dkt. Abbasi alieleza kuwa mafanikio hayo ni zao la juhudi za viongozi mbalimbali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania, pamoja na ushiriki wa mabalozi, taasisi na wadau katika maonesho makubwa ya utalii kimataifa.

“Mbegu hizo ndizo zimezaa mavuno haya. Na sasa tunaangalia mbele zaidi – kutangaza nchi kwenye majukwaa makubwa kama michezo na matamasha yanayovuta macho ya dunia, kama ilivyo kwa Qatar na Saudia,” alifafanua Dkt. Abbasi.

Watalii Wafurika, Mapato Yavunja Rekodi

Akijibu kuhusu iwapo takwimu hizo zinalingana na hali halisi nchini, Dkt. Abbasi alisema, “Nchi imefurika watalii kila kona. Taarifa ya Benki Kuu (BoT) ya hivi karibuni inaonesha utalii umeingiza dola bilioni 3.92 – ikishika nafasi ya kwanza kwa kuchangia fedha za kigeni.”

Aliongeza kuwa taasisi kubwa za utalii kama TANAPA, TFS, TAWA na Mamlaka ya Ngorongoro zimekusanya mapato kwa kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu zianzishwe.

Akitolea mfano masoko makuu ya nje, Dkt. Abbasi alitaja Marekani kuwa na ongezeko la watalii kwa asilimia 41, huku China na India zikionesha ongezeko kubwa zaidi, China kwa asilimia 108 na India asilimia 75.

“Kwa kifupi, kona zote tunaona watalii wanaongezeka na mapato yanapanda. Narudia tena na shika sana hili neno MIKAKATI,” alisisitiza.



Chapisha Maoni

0 Maoni