Katika kuwajengea uwezo wazalishaji wa chimvi nchini,Serikali imekuja na mikakati mbalimbali kufikia azma hiyo ikiwemo upunguzaji wa ada ya pango kwa mwaka ya leseni (Annual Rent) za uchimbaji mdogo wa chumvi nchini ili kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuchochea uzalishaji wa wingi wa chumvi nchini.
Hayo yamesemwa jana
tarehe 15 Julai, 2025 na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb)
Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga Kikao cha wadau wa sekta ndogo ya
chumvi chini ya Chama cha Wazalishaji wa Chumvi Tanzania (TASPA).
"Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutubeba sekta ya madini na wachimbaji kwa
ujumla. Ni yeye aliyetuelekeza kusikilize kilio chenu na kutatua changamoto
zinazowakabili ili mnufaike na shughuli mnazofanya."
"Ametuelekeza Wizara
ya Madini tuliridhie ombi lenu na kupunguza ada ya pango ya mwaka ya leseni ya
uchimbaji mdogo kutoka Shilingi 45,000 mpaka Shilingi 20,000 kwa hekta, hili
linakwenda kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ubora wa chumvi ya
mzalishaji mdogo," alieleza Mhe. Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde
alibainisha kuwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ikiwemo udhibiti
wa chumvi inayoingizwa kutoka nje ya nchi, zimepelekea bei ya chumvi ghafi
kuongezeka na hivyo kuwanufaisha zaidi wazalishaji wadogo wa chumvi nchini.
Uanzishwaji wa kodi ya
zuio ya asilimia mbili (2%) kwenye mauzo ya chumvi ghafi kwa wazalishaji wenye
leseni za PML imekuwa ni neema na manufaa kwao badala ya utaratibu wa awali wa
kufanyiwa makadirio ya kodi ya mapato, ambao ulikuwa ni kero kubwa kwa
wazalishaji wadogo.
Katika hatua nyingine,
Mhe. Mavunde alieleza kuwa Kiwanda cha kuzalisha chumvi cha STAMICO kipo hatua
za mwisho, na kuagiza Shirika hilo kuhakikisha kabla ya mwezi wa Agosti kuisha
kiwe kimekamilika na kuanza uzalishaji wa chumvi ili kupanua wigo wa soko la
chumvi ya wazalishaji wadogo.
Awali, akitoa taarifa ya
utendaji wa Taasisi yao, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Chumvi Tanzania
(TASPA), Bi. Hawa Ghasia aliishukuru Serikali kwa kushughulikia changamoto
zilizokuwa zinaikabili sekta ndogo ya chumvi nchini ambazo zimepelekea bei ya
chumvi kupanda na kuwanufaisha zaidi wazalisha chumvi nchini.
0 Maoni