Naibu Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Prof. Tumaini Nagu,
amewakumbusha na kuwataka Makatibu Tawala wa Mikoa, Maafisa Lishe na Maafisa
Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu Programu ya Kitaifa ya
Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECDI 2030) ili kuwawezesha
watoto kukua katika mazingira bora na kuzifikia ndoto zao.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa kikao kazi cha uwasilishaji wa viashiria vya malezi, makuzi na
maendeleo ya awali ya mtoto kilichofanyika leo Julai 2, 2025 Jijini Dodoma,
Prof. Nagu amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa programu hiyo kuanzia ngazi ya
Mkoa hadi ngazi ya jamii.
“Ndugu washiriki,
natumia fursa hii kuwakumbusha kwenda kutekeleza kikamilifu programu hii ya
kitaifa ili kuwawezesha watoto wetu kukua na kufikia utimilifu wao, ndoto zao
zitimie na waweze kuwa na mchango mkubwa kwa taifa letu,” alisema Prof. Nagu.
Ameongeza kuwa ni
muhimu kwa Mikoa na Halmashauri zote kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya
kuchochea utekelezaji wa programu hiyo katika maeneo yao.
Awali, Mwakilishi wa
Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), Bwana Abbas Mtemba, alieleza kuwa
kama Taifa bado kuna changamoto kubwa ya kuhakikisha watoto wote wanapata fursa
sawa za ukuaji wa kiafya, kielimu, kiakili na kijamii.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto
(TECDEN), Bi. Mwajuma Kibwana, aliwasilisha takwimu za kitaifa zinazoonesha
kuwa asilimia 47 pekee ya watoto wenye umri wa miezi 24 hadi 59 walio katika
hatua ya ukuaji timilifu, huku asilimia 53 wakiwa bado wanakumbwa na changamoto
mbalimbali katika malezi na makuzi yao.
Kikao kazi hicho
kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makatibu Tawala wa Mikoa kutoka
Mikoa 15, Maafisa Lishe wa Mikoa na Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka maeneo
mbalimbali nchini.
Na. OR - TAMISEMI



0 Maoni