Idadi ya watu
waliopoteza maisha katika ajali ya mabasi mawili kugongana na baadaye kushika
moto wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, imeongezeka na kufikia 42, kutoka 39
vilivyoripotiwa awali.
Akizungumza na
waandishi wa habari Jumatano, Julai 2, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Nurdin Babu, amesema kuwa kati ya waliopoteza maisha, 31 walikuwa wakisafiri
katika basi dogo aina ya Coaster, huku wengine 11 wakiwa kwenye basi kubwa.
Kuhusu hali ya
majeruhi, mkuu huyo wa mkoa amesema jumla ya watu 24 waliokuwa wamelazwa tayari
wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya hali zao kuimarika, huku majeruhi wawili
wakiendelea kupokea matibabu hospitalini.
Mkuu huyo pia amesema
kuwa miili saba kati ya ile iliyonusurika kuteketea vibaya imetambuliwa na
ndugu zao bila ya kuhitaji vipimo vya vinasaba (DNA), na tayari taratibu za
Mazishi zimefanyika.
“Tunatarajia kupata
majibu kamili ya vipimo vya DNA ifikapo jioni ya leo, jambo ambalo litatoa
fursa kwa ndugu wa waathirika kuweza kuwatambua wapendwa wao waliopoteza maisha,”
amesema.
Ajali hiyo iliyotokea
tarehe 28 Juni , 2025 imehusisha jumla ya abiria 67, ambapo 64 walikuwa watu
wazima na watoto watatu.
Hata hivyo imebainika
kuwa Chanzo Cha kutokea ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi la mbele la basi kubwa
la abiria kampuni ya Chaneli one jambo lililopelekea dereva
kukosa mwelekeo.


0 Maoni