WAZIRI MKUU, na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa Kassim Majaliwa leo Julai 2, 2025 ametangaza rasmi kutokugombea tena ubunge wa jimbo la Ruangwa baada ya kulitumikia jimbo hilo kwa miaka 15.
Akizungumza na
wajumbe wa kamati ya Siasa ya Mkoa na Wilaya ya Ruangwa Mheshimiwa Majaliwa
ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi kwa kumuunga mkono wakati wote ambao
amekuwa mbunge wa jimbo hilo.
"Imefika wakati
kwa mshikamano tulioujenga sasa ni wakati wa kutoa fursa kwa
Wana-Ruangwa wengine wapenda maendeleo waweze kuunganisha nguvu hizi ili Kauli
mbiu yetu ya Ruangwa kwa maendeleo inawezekana iweze kusonga mbele zaidi."
Aidha, ametoa wito
wajumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya kuwapa ushirikiano wagombea wote wenye nia
ya kugombea ubunge wa jimbo hilo.
Kadhalika, Mheshimiwa
Majaliwa amewasihi Wana-Ruangwa kuendelea kushikamana na itakapofika siku ya
uchaguzi waweze kuchagua wagombea wote watakaowakilisha chama cha Mapinduzi
kwenye uchaguzi huo.
"viongozi wetu
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza Dkt. Nchimbi watakapokuja
tujitokeze kwa wingi kwenye mikutano tusikilize sera, lakini siku ya kupiga
kura tuwapigie kura nyingi za kutosha."
Aidha, amemshukuru
Rais Dkt. Samia Viongozi wakuu wa chama cha Mapinduzi (CCM) kwa
kumuamini na kumpa fursa ya kuwatumikia wana Ruangwa.
Mheshimwa Majaliwa
alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Ruangwa mwaka 2010 na amehudumu kwa
kipindi cha miaka 15.



0 Maoni