Mkurugenzi Msaidizi
wa huduma za Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi. Subisya Kabuje
amesema Serikali imedhamiria kusogeza huduma za Ustawi kwa Jamii kwa Wananchi
hasa wale waliopo katika mazingira hatarishi na wanaokuMbwa na changamoto za
kijamii.
Bi. Kabuje ameyasema
hayo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI katika halfa ya
Uzinduzi wa Madawati ya huduma za Ustawi wa Jamii katika vituo vya usafirishaji
Nchini na uzinduzi wa Kiongozo cha Taratibu na Utoaji wa Huduma za Ustawi wa
Jamii Kwa Watoto wanaoishi na kufanya Kazi mitaani iliyofanyika katika stendi
ya Magufuli Jijini Dar es Salaam.
“Dawati hili ni
kielelezo cha utayari wa Serikali kusogeza huduma za kijamii karibu zaidi na
wananchi hasa wale walio katika mazingira hatarishi kama Watoto waliopotea ama
kutoroka familia zao, Watoto ambayo ni wahanga wa biashara haramu ya
usafirishaji wa binadamu na wahanga wa vitengo vya kikatili na kijinsia waliopo
safarini,” alisema Bi. Kabuje.
Amesema Ofisi ya Rais
TAMISEMI Kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na
Makundi Maalum inaendelea kusimamia madawati hayo na kuhakikisha yanaungwa
mkono katika Halmashauri zote.
Naye, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dorothy Gwajima amewataka Wazazi na Walezi kutekeleza wajibu na majukumu yao kwani Serikali imeweka Mifumo mbalimbali ili kupambana na changamoto ya Watoto wa wanaoishi mazingira hatarishi.
“Serikali imeweka
Mifumo mbalimbali ya kusababisha Jambo hili lisitokee lakini Jambo hili
linatokea kwasababu baadhi ya Wazazi na Walezi hawatimizi wajibu wao kikamilifu
katika malezi ya Watoto,” alisema Mhe. Gwajima.
Amesema Kiongozo
hicho ambacho kimezinduliwa kitasaidia katika kuongoza kwenye huduma za vituo
vya usafirishaji na kubaini mapema viashiria vya hatari vya ukatili.
Madawati haya ya
huduma za Ustawi wa Jamii katika vituo vya usafirishaji yamezinduliwa katika
Mikoa 11 nchini ambapo hadi sasa kuna jumla ya madawati 14 ambayo wanawezeshwa
na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Railway Children Africa.
Na. OR TAMISEMI



0 Maoni