Serikali kupitia Wakala
wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) leo
tarehe 22 Julai, 2025 wamesaini mkataba wenye lengo la kujenga kiwanda kipya
cha kuzalisha nishati mbadala (Mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes) mkoani Geita
ambapo mkataba huo una thamani ya shilingi bilioni 4.5.
Katika hafla iliyofanyika
katika Ofisi ndogo ya REA, Jijini, Dar es Salaam, REA itatoa jumla ya shilingi
bilioni tatu na STAMICO itatoa shilingi bilioni 1.5; kwa mchanganuo huo, REA
itagharamia ununuzi wa mtambo wakati STAMICO italipia upatikanaji wa kiwanja,
ujenzi wa jengo la kiwanda na gharama za ufungaji wa mitambo.
Mkataba huo umesainiwa na
Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu wa REA pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa
STAMICO, Dkt. Venance Mwasse.
Mkataba huo utaifanya
STAMICO kuwa na viwanda vikubwa vitano vya kuzalisha mkaa mbadala wa Rafiki
Briquettes; viwanda vingine ambavyo vinaendelea na uzalishaji wa mkaa mbadala
vipo wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani, Kiwira mkoani Songwe, na viwanda vingine
viwili vipo mkoani Dodoma na Tabora ambapo vipo kwenye hatua za mwisho za
ukamilishwaji kabla kuanza uzalishaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi, Hassan Saidy,
amesema kuwa Wakala umepewa jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi
ya kupikia unafikia asilimia 80 kwa Watanzania wote ifikapo mwaka 2034.
“Katika kufanikisha lengo
hilo, Wakala unatekeleza Miradi mbalimbali ikiwemo uwezeshaji katika kuongeza
uzalishaji na usambazaji ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia
kwa Watu wa vijijini.”
“Utiaji wa saini wa
Mkataba huo kati ya REA na STAMICO ni moja wapo ya utekelezaji wa maagizo ya
Mheshiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
Wakala ili kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa kuona namna ya kuongeza uzalishaji
na upatikanaji wa nishati safi kwa Wananchi ili waondokane na matumizi ya
nishati zisizo safi na salama,” amesema Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu
REA.
“Ni matumaini yetu kuwa
Mkataba huu utaende kuongeza kasi ya upatikaji wa mkaa mbadala na kwa bei nafuu
ikiwa ni mojawapo ya lengo la Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia. Tunatambua
kuwa utunzaji wa mtambo huu ni muhimu sana ili huduma iliyokusudiwa iendelee
kutolewa kwa wakati bila kuathili uchumi wa Wananchi, afya na pamoja na
mazingira kwa ujumla,” amekaririwa, Mhandisi, Hassan Saidy.
Mhandisi, Saidy ameongeza
kuwa Wakala unaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali ili kuhakikisha Mkakati
wa Nishati safi ya kupikia unatimiza malengo yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na
kuongeza upatikanaji na usambazaji wa mkaa mbadala, Wakala unaendelea
kutekeleza Miradi mbalimbali ikiwemo usambazi wa majiko banifu, usambazaji wa
majiko ya umeme, usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia majumbani (LPG ya
kilo 6 na 15); usambazaji wa gesi asilia katika mkoa wa Lindi na Pwani pamoja
na ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika Taasisi za Umma.
Kwa upande wake, Dkt.
Venance Mwasse, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO ameishukuru Serikali kupitia REA
kwa mchango huu ambao utasaidia Shirika hilo
kutimiza ndoto yake ya kuhakikisha wananchi wote wanaachana na nishati
isiyo safi na salama ya kupikia ifikapo mwaka 2034 na hivyo kuunga mkono juhudi
za Serikali za kutunza mazingira.
“Hii ajenda ya matumizi
ya nishati safi ambayo kinara wake ni Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu
Hassan inalenga kumkomboa Mwanamke ili aachane na nishati isiyo safi na salama.
STAMICO tumejipanga kutekeleza maono haya ya Kiongozi wetu,” amesema Dkt.
Mwasse.
Ameongeza kuwa nishati ya
Rafiki Briquettes kwa sasa inatumiwa na Jeshi la Magereza ambapo Magereza yote
129 nchini kote yanatumia nishati hii kama aina mojawapo ya nishati ya kupikia,
vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT).
Taasisi nyingine ni
pamoja na vyuo mbalimbali vya mafunzo, shule za msingi na sekondari, hoteli,
migahawa, na sehemu wanazochoma nyama na chipsi.
Dkt. Mwasse amesisitiza
kuwa STAMICO itaendelea kutunza mitambo hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa
Wananchi.

0 Maoni