Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anapenda kufanya kazi na viongozi wa dini kwa kuwa
anawaongoza wananchi wenye dini ambao dini zao wanaziheshimu na hivyo
asingependa kuona haki zao zinanyimwa kwa namna yoyote ile.
Dkt. Biteko amesema
hayo Julai 3, 2025 jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
Mkutano Mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).
“Mheshimiwa Rais
Samia anapenda kufanya kazi na viongozi wa dini na ninyi ni mashahidi amekuwa
akiwaalika ili tuzungumze masuala mbalimbali ya kitaifa ingekuwa ni mtu anayejifungia ndani na akasema analo
jeshi, sheria, katiba na vyombo vya ulinzi basi nitafanya kazi nadhani hivi
ingekuwa ngumu sana lakini yeye amesema
milango yetu iwe wazi tuzungumze na viongozi
wa dini kwa ajili ya kutafuta mustakabali wa nchi yetu pale ambapo tunadhani hatuendi sawasawa,” amesema Dkt.
Biteko.
Akijibu hoja za CCT,
Dkt. Biteko amesema kuwa imekuwa desturi ya nchi kuwa na waangalizi wa ndani
kwenye Uchaguzi Mkuu na kuwa ni imani yake kuwa Tume Huru ya Uchaguzi itawalika waangalizi wa ndani ikiwa ni pamoja
na asasi za kiraia. Hata hivyo amesisitiza Tume Huru ya Uchaguzi iachiwe uhuru
wake wa kufanya kazi zake.
Amewahakikishia kuwa
Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na taasisi zote za dini
ikiwemo makanisa na kusema kuwa tangu Uhuru mwaka 1961, Taasisi za dini
zimeendelea kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuwanufaisha watu
wengi kote nchini.
“Tunawapongeza sana
na tunawashukuru sana kwa mchango wenu. Tafiti zinaonesha kuwa Taasisi za dini
Barani Afrika huchangia kati ya asilimia30 hadi 70 ya maendeleo ya sekta ya
afya. Kidunia, kwa mfano katika elimu, Vyuo kama University of Edinburgh - (Scotland),
Oxford University - Uingereza na University of Kwa Zulu - Natal Afrika ya
Kusini vilianzishwa na Taasisi za dini,”
amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea
kuzungumzia mchango wa taasisi za dini katika kuzalisha wataalamu wa fani
mbalimbali duniani ambao wanaendelea kuiokoa dunia kutoka katika matatizo na
majanga mbalimbali akitolea mfano Tasisi
ya World Coucil of Churches na World Vision kwa kutoa huduma za kibinadamu
duniani kote bila kubagua tofauti zilizopo za dini, rangi, kabila na jinsia.
Katika kutambua
mchango wa viongozi wa dini Afrika na duniani kote, Dkt. Biteko ameelezea haiba
ya Mwanatheolojia Muanglikana kutoka Afrika Kusini, Hayati Baba Askofu Desmund
MpiloTutu kama kiongozi wa dini mwenye upendo, mpendahaki na amani, ambaye amechangia
kutetea haki za binadamu na kupambana dhidi ya u baguzi na hivyo kusaidia
kuleta maendeleo na usawa kwa nchi ya Afrika Kusini na dunia kote.
Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Kikistro Tanzania, Baba Askofu, Dkt. Fredrick Shoo amepongeza usikivu wa
Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na juhudi za Serikali za kudumisha
demokrasia kwa kuruhusu mikutano ya hadhara sambamba utekelezaji wa miradi ya
maendeleo nchini.
Katika kuelekea
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Baba Askofu Dkt. Shoo amesema CCT inahimiza maadili
ya kisiasa na utulivu wa jamii ikiwa ni pamoja na kampeni zisizo za kuvunjiana
heshima bali zinazoweka mbele maslahi ya Taifa na kupinga vitendo vyote vya
rushwa.
“ Uchaguzi ni daraja
la amani na maendeleo si chanzo cha mifarakano, jamii idumishe amani,
mshikamano na uzalendo wa kila mmoja kwa nafasi yake. Pia Tume Huru ya Uchaguzi
iendelee kusimamia haki kwa kushirikiana na waangalizi wa ndani amesema ,” Baba
Askofu Shoo.
Amebainisha kuwa CCT
itaendelea kushirikiana na Serikali kuleta maendeleo ya jamii hivyo ameiomba
Serikali itoe unafuu wa kodi na kutotoza ruzuku kwa misaada inayotolewa na
wahisahi ili kuboresha ubora wa huduma na kuwafikia wananchi.
Katibu wa Jumuiya ya
Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Dkt. Moses Matonya amesema kuwa CCT ni Jumuiya
inayounganisha madhehebu wanachama 12 na
mashirika ya kikristo 14. Aidha katika Mkutano huo jumla ya wajumbe waliohudhuria ni 224 kati ya wajumbe wote 280.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akisalimiana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikistro Tanzania, Askofu. Dkt. Fredrick Shoo wakati alipowasili kwenye Ufunguzi wa Mkutano Mkutano Mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) uliofanyika Julai 3, 2025, Jijini Dodoma.
Na. Ofisi ya Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni