Serikali ya Tanzania
imekanusha vikali tuhuma zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinazodai kuwa
kuna mpango wa kumwekea sumu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Tundu Antipas Lissu, ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi mahakamani.
Kupitia taarifa
iliyotolewa leo na Idara ya Habari (MAELEZO), Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw.
Gerson Msigwa, amesema tuhuma hizo hazina msingi wowote na kwamba Serikali
haina mpango wala dhamira ya kufanya jambo la namna hiyo.
"Serikali
inawaomba wananchi kupuuza taarifa hizo kwa kuwa si za kweli na zinalenga
kupotosha umma," alisema Msigwa katika taarifa hiyo.
Amefafanua kuwa
Lissu, ambaye ametajwa kwenye taarifa hizo pamoja na kauli za baadhi ya
wanasiasa wa nje ya nchi, kwa sasa yupo gerezani kwa mujibu wa sheria,
akisubiri shauri lake kukamilika mahakamani.
Msemaji huyo
amesisitiza kuwa Serikali haijawahi kuwa na mpango wa kumuwekea sumu mfungwa
yeyote na wala haina nia ya kufanya hivyo kwa mtu yeyote anayeendelea
kushikiliwa kwa mujibu wa sheria.
Amesema kusambazwa
kwa taarifa hizo ni sehemu ya njama za kuharibu taswira ya nchi kimataifa na
kuchafua heshima ya Tanzania, ambayo imejijengea sifa ya kuheshimu haki, sheria
na taratibu.
"Tayari mamlaka
zinazohusika zimeanza kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika kuchapisha na
kusambaza uongo huu," imeeleza taarifa hiyo.
Serikali imetoa wito
kwa wananchi kuwa na subira na kuendelea kuiamini mifumo rasmi ya utoaji wa
taarifa huku ikiweka wazi kuwa haitavumilia upotoshaji unaolenga kuchochea hofu
au kuleta taharuki kwa jamii.


0 Maoni