Baada ya kukamilika
kwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi za ubunge na
udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), sasa mchakato unahamia katika hatua
nyingine muhimu ya kuchambua na kupendekeza majina ya wagombea.
Kuanzia kesho, Julai
4, 2025, kamati za siasa katika ngazi mbalimbali zinaanza vikao maalumu kwa
ajili ya kuwajadili wanachama waliotia nia ya kugombea nafasi hizo, kabla ya
kupitishwa kwa majina ya mwisho katika ngazi ya taifa.
Kwa mujibu wa ratiba
rasmi iliyotolewa na CCM, vikao vya kamati za siasa za kata na wadi vitaanza
kesho kwa ajili ya kuwajadili wagombea wa nafasi ya udiwani wa kawaida pamoja
na wa viti maalumu. Baada ya uchambuzi huo, mapendekezo yatapelekwa kwenye
kamati za siasa za ngazi ya jimbo kwa upande wa Zanzibar na wilaya kwa upande
wa Tanzania Bara.
Vikao hivyo
vitaendelea Julai 5, 2025, ambapo kamati za siasa za majimbo kwa upande wa
Zanzibar zitawajadili wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi.
Mapendekezo ya vikao hivyo yatapelekwa kwa kamati za siasa za wilaya kwa hatua
zaidi.
Hatua hii ni sehemu
ya mchakato mpana wa ndani wa chama unaolenga kuhakikisha upatikaji wa wagombea
wenye sifa, uadilifu na uwezo wa kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.

0 Maoni