Makalla ampongeza Majaliwa kwa uamuzi kutowania ubunge Ruangwa

 

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla, amempongeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa uamuzi wake wa busara wa kuahirisha kuchukua fomu ya kuwania ubunge katika Jimbo la Ruangwa, mkoani Lindi.

Akizungumza leo Julai 3, 2025, jijini Dar es Salaam, Makalla amesema uamuzi huo unaonyesha ukomavu wa kisiasa na unafungua fursa kwa vijana wengine wa Ruangwa kuendelea kuchangia maendeleo ya jimbo hilo kupitia nafasi ya ubunge.

“Kwa kweli tumpongeze Waziri Mkuu Majaliwa. Amefanya kazi nzuri sana. Awamu ya tano alifanya kazi nzuri na marehemu Dkt. John Pombe Magufuli, na pia amefanya kazi nzuri na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hakika, Mheshimiwa Majaliwa amefanya kazi kama mtu aliyekuwa madarakani kwa vipindi viwili,” alisema Makalla.

Makalla aliongeza kuwa Majaliwa ameamua kwa hiari yake kutogombea tena ubunge, akitambua kuwa ameshatimiza wajibu wake kwa Taifa kama Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka 10, na sasa ni wakati wa kuwapa nafasi wengine kuendeleza kazi hiyo.

“Kwangu mimi huu ni uamuzi wa hekima. Ni uamuzi unaoonyesha busara na unastahili kuungwa mkono. Amelihudumia vyema jimbo lake la Ruangwa, ametumikia Watanzania kwa bidii, na sasa ameona ni wakati sahihi kusema ‘panatosha’,” aliongeza.

Makalla pia alitumia nafasi hiyo kumpongeza Majaliwa kwa mchango wake katika maendeleo ya jimbo la Ruangwa, akitolea mfano mafanikio ya timu ya Namungo FC ambayo kwa sasa inashiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ikiwa ni miongoni mwa mafanikio ya kiuongozi katika eneo hilo.

“Ameiacha Ruangwa ikiwa imara, Namungo ipo Ligi Kuu, na haya ni miongoni mwa matunda ya uongozi wake. Huu ni uamuzi wa busara na sisi kama chama tunampongeza kwa moyo wake wa kujitoa kwa ajili ya Taifa,” alisisitiza Makalla.

Chapisha Maoni

0 Maoni