Baadhi ya wananchi kutoka
Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani wamejitokeza kwa wingi kutembelea vivutio vya
kihistoria katika mji mkongwe wa Bagamoyo, wakichochewa na elimu na ofa maalum
ya utalii waliyoipata kupitia Banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba.
Wakazi hao waliotembelea
maeneo ya kihistoria wamesema elimu waliyoipata imewafungua macho kuhusu
thamani ya utalii wa ndani na umuhimu wa kuhifadhi urithi wa taifa, huku
wakieleza furaha yao baada ya kujionea vivutio hivyo kwa macho.
Agness Shayo, mmoja wa
wageni waliotembelea Banda la TFS Sabasaba, alisema alihamasika kuja Bagamoyo
baada ya kusikia simulizi za vivutio vya kipekee.
“Nilipoelezwa kuhusu
Mbuyu wa Ajabu ambao ukiuzunguka unaongeza siku za kuishi, nilitamani sana
kuona. Sasa nimeona kwa macho yangu na hata kushuhudia Kisima cha Miujiza
ambacho hakikauki maji,” alisema Shayo kwa furaha.
Kwa upande wake, Brigiti
Mahanga, mwanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana St. Alicia iliyoko
Visiga, alisema ziara hiyo imeongeza uelewa wake kuhusu historia.
“Tunaambiwa sana kuhusu
historia darasani, lakini kujionea kwa macho kunasaidia kuelewa zaidi.
Ningependa wanafunzi wengi wapate fursa kama hii,” alisema na kuomba vivutio
hivyo vilindwe kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Akizungumzia ongezeko la
wageni msimu huu, Mhifadhi wa Eneo la Kaole, Bi Siyawezi Hungo, alisema
kumekuwa na ongezeko la Watanzania wanaotembelea vivutio vya Bagamoyo hasa
msimu wa Sabasaba, jambo linalodhihirisha mwamko mpya wa kuthamini utalii wa
ndani.
“Watu wanapenda kujua
historia yao na sasa tunashuhudia wengi wakifika kujifunza na kushangaa urithi
huu wa zaidi ya miaka 800 iliyopita,” alisema Bi Siyawezi.
Magofu ya Kaole na Mji
Mkongwe wa Bagamoyo umeendelea kuwa kitovu cha historia na urithi wa
kiutamaduni nchini, kutokana na vivutio kama Kaburi la Wapendanao, Msikiti wa
kale wa zaidi ya miaka 800, Mbuyu wa Ajabu na Kisima cha Miujiza, ambavyo
vimekuwa kivutio kwa watalii wa ndani na wageni kutoka nje ya nchi, hasa wakati
wa matukio makubwa ya kitaifa kama Sabasaba.
0 Maoni