Maandalizi ya hafla ya uzinduzi wa Dira 2050 yakamilika

 

Maandalizi ya hafla kubwa ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050) yamekamilika rasmi, ambapo hafla hiyo inatarajiwa kufanyika Julai 17, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Mrisho Kikwete, Jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Meneja wa Mawasiliano Serikalini kutoka Tume ya Taifa ya Mipango (NPC), Bw. Titus Kaguo, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya uzinduzi huo yamekamilika kwa asilimia mia moja.

Hafla hiyo ya uzinduzi wa Dira 2050, inayobeba kaulimbiu ya “Tanzania Tuitakayo 2050”, inatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya wananchi 5,000 kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia atazindua rasmi Dira hiyo ambayo inatazamiwa kuwa mwongozo wa maendeleo ya taifa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.

Kaguo amesema kuwa Dira 2050 imeandaliwa kwa ushirikiano wa karibu na wadau kutoka sekta mbalimbali, ambao walitoa maoni yao kuhusu aina ya Tanzania wanayoitamani ifikapo mwaka 2050.

“Maoni ya wananchi na wadau mbalimbali ndiyo msingi wa Dira hii mpya. Hii ni Dira ya Watanzania wote, inayolenga kujenga taifa lenye uchumi imara, jamii jumuishi, na ustawi kwa wote,” amesema Kaguo.

Uzinduzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu katika safari ya maendeleo ya Tanzania, huku ukiweka mkazo katika ustawi wa kijamii, uchumi jumuishi, maendeleo ya rasilimali watu, matumizi ya teknolojia, na utunzaji wa mazingira.

Chapisha Maoni

0 Maoni