RC Sendiga awataka wafanyabiashara Manyara kuwekeza kwenye miradi mikubwa

 

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amewahimiza wafanyabiashara wa mkoa huo kujielekeza katika uwekezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, akisema kuwa mkoa wa Manyara unakua kwa kasi na unahitaji mchango wao katika kukuza uchumi.

Akizungumza jana Septemba 2, 2025, wakati wa kufungua Baraza la Kumi na Moja la Wafanyabiashara wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Sendiga alisema tayari mazingira ya uwekezaji yameandaliwa na kuna miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo mradi wa TACTIC wenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 19.

“Kikao cha mwisho tulikubaliana hapa, Mkurugenzi wa Mji wa Babati alisema yapo maeneo ambayo tayari yameshatengwa kwa ajili ya uwekezaji. Mnaona, mradi wa TACTIC umeanza juzi, wa zaidi ya bilioni 19 tumepata hapa,” alisema Mhe. Sendiga.

“Tujenge nyumba za wageni, tujenge migahawa, watu wa mabenki wapeni watu mikopo. Tunakwama wapi wafanyabiashara ? Sisi tunataka mkoa ukue.”

Aidha, aliwahimiza wafanyabiashara waliokutana katika baraza hilo kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo maazimio na mapendekezo yote yaliyotolewa, huku akibainisha kuwa mkoa umeshajipanga kwa kuzindua timu maalumu kwa ajili ya kuratibu masuala ya uwekezaji.

Mkuu huyo wa mkoa pia alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuimarisha mazingira ya biashara nchini, ikiwemo kuboresha miundombinu na kurahisisha taratibu za kufanya biashara.

“Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa mipango madhubuti na ya makusudi ya kuhakikisha kwamba miundombinu ya biashara inakuwa rafiki, na ufanyaji wa biashara unakuwa mwepesi,” aliongeza Mhe. Sendiga.

“Hii inasaidia hata mtu anayepata faida ndogo kuweza kuiona na kunufaika nayo.”

Katika hatua nyingine, alizitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo kuhakikisha wanakusanya mapato kwa kuzingatia uhalisia wa mazingira ya biashara, huku akishauri kufanyika kwa mapitio ya makadirio ya kodi ili yaendane na hali halisi ya wafanyabiashara.

                   Na. Ruth Kyelula - Manyara RS

Chapisha Maoni

0 Maoni