Katibu wa Halmashauri Kuu
ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), CPA
Amos Makalla, amesema hadi sasa hakuna mwanachama yeyote aliyeenguliwa katika
mchakato wa kuomba kugombea nafasi za Udiwani au Ubunge.
Akizungumza na waandishi
wa habari leo Julai 13, 2025 katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM Jijini Dodoma,
Makalla amesema taarifa zinazoenezwa kuwa baadhi ya wagombea wameenguliwa si za
kweli na zinalenga kupotosha umma kuhusu mchakato wa ndani ya chama hicho.
“Naomba nisisitize, kwa
utaratibu wetu wa Chama cha Mapinduzi, mpaka sasa hakuna mtu ambaye ameenguliwa
au kukatwa kama ambavyo inaripotiwa kwenye vyombo vya habari. Nimeona
wameandika huyu kapenya, huyu kafyekwa, huyu hayupo kwenye tatu bora... lakini
mchakato huu bado unaendelea,” amesema Makalla.
Amefafanua kuwa kwa sasa
Sekretarieti ya CCM inaendelea kupokea taarifa kutoka mikoa mbalimbali, na
taarifa hizo zitawasilishwa kwenye vikao vya juu vya chama, likiwemo la Kamati
Kuu ambako maamuzi ya mwisho yatafanyika.
Makalla amesema kwamba ni
Kamati Kuu ya CCM pekee ndiyo yenye mamlaka ya kutoa orodha rasmi ya wagombea
watakaokwenda kupigiwa kura za maoni.
“Kamati Kuu
itakapohitimisha, tutatoka kuwaambia walioteuliwa kwenda katika kura za maoni
ndani ya CCM. Zamani mlivyozoea ni kwamba kila mgombea alikuwa anapelekwa
kwenye kura za maoni, lakini sasa tunachuja na kupitisha wachache tu kwa ajili
ya kura hizo,” amesema.
Amesisitiza kuwa mchakato
huo unazingatia taratibu za chama, na kuwahakikishia wanachama wote kuwa haki
na usawa vitazingatiwa hadi mwisho wa mchakato huo.
0 Maoni