WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa madhehebu ya dini nchini kuendelea
kuihimiza jamii kuzingatia msingi ya maadili na kuepuka mienendo iliyo kinyume
na tamaduni, mila na desturi ya Mtanzania
Amesema kuwa moja ya eneo
ambalo viongozi hao wanapaswa kukemea ni kuhusu
matumizi, biashara na usambazaji wa dawa za kulevya kwani kwa kufanya
hivyo kutasaidia kunusuru maisha ya Watanzania hususan vijana.
Amesema hayo leo
(Jumapili, Julai 13, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
ibada ya kumweka wakfu na kumuingiza kazini Askofu Mteule Dkt. Daniel Henry
Mono wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mwanga, mkoani
Kilimanjaro.
“Tuendelee kupambana
vikali na matumizi ya dawa za kulevya sababu athari yake ni kubwa hasa kwa
vijana wetu, vijana ni kundi tegemewa, matumizi ya dawa za kulevya yanaharibu
uelewa na afya za vijana wetu.”
Mheshimiwa Majaliwa
amesema Serikali kwa upande wake imeendelea kuweka sheria kali pamoja na
kuimarisha ukaguzi wa kubaini uingizaji wa dawa za kulevya nchini. “Tupo imara
usikubali kushiriki katika biashara hii”.
Katika hatua nyingine,
Mheshimiwa Majaliwa ameyapongeza madhehebu ya dini ikiwemo Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika
kuihudumia jamii ya Watanzania.
“Serikali itaendelea
kushirikiana na madhehebu ya dini katika kufanikisha masuala mbalimbali
yanayounganisha Taifa letu ikiwemo Agenda za kitaifa, kuimarisha masuala ya
maadili na kujenga jamii inayozingatia misingi ya kudumisha upendo, amani na
utulivu.”
Ameongeza kuwa madhehebu
hayo yamekuwa yakitoa mchango mkubwa katika kutoa huduma za afya, elimu, malezi
ya vijana, utunzaji wa mazingira pamoja na huduma kwa makundi maalum yenye
uhitaji ikiwa ni kuinga mkono Serikali katika kutoa huduma.
Kadhalika, Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa Serikali wakati wote itaendelea kufanya kazi na
kushirikiana na madhehebu ya dini nchini kwa ajili ya manufaa ya watanzania
wote.
Pia, Waziri Mkuu amesema
Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia itaendelea kufanya kazi usiku na
mchana ili kuimarisha ustawi wa wananchi katika nyanja zote za utoaji huduma
pamoja na kusimamia uwepo wa Amani na Utulivu katika jamii.
Aidha, Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 488 kwa
ajili ya upanuzi wa barabara ya nia nne kuanzia Mailisita, Kiboriloni hadi
Holili.
Mheshimiwa Majaliwa
amepongeza Baba Askofu Mteule Dkt. Mono kwa kupewa nafasi ya kuiongoza Dayosisi
ya Mwanga ambapo amesema uteuzi wake ni ishara kuwa amekidhi vigezo na
kustahili kupewa daraja hili kubwa katika jamii.
“Ninakupongeza sana kwa
kuwa umethibitika mbele ya Mungu na wanadamu, nafasi ya Askofu ni kubwa kwenye
kanisa kwa kuwa askofu ni msimamizi wa kanisa. Kwa maneno mengine wewe ndiye kiongozi
wa kiroho wa washarika wote wa Mwanga, hili ni jukumu kubwa sana ambalo
unapaswa kulitekeleza kwa hekima kuu”.
Naye Askofu Mteule Dkt.
Daniel Henry Mono ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuliombea Taifa hasa
katika kipindi cha kuendelea uchaguzi mkuu utakaofanyika Mwezi Oktoba 2025 ili
haki na amani viweze kudumua na mapenzi ya Mungu yaweze kutimia kwa kupata
viongozi watakaoongoza kwa maslahi ya Taifa zima.
Ameongeza kuwa Dayosisi
hiyo itaendelea kushirkiana na Serikali kama mdau mkubwa na mshirika wa karibu
wa kanisa bila kuathiri misingi ya imani na kanisa.
0 Maoni