Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini TANAPA - Jenerali Mstaafu George Waitara amewahamasisha wawekezaji
kuwekeza katika mazao ya utalii pamoja na malazi hususani katika Hifadhi za
Kusini zilizojaliwa kuwa na hazina lukuki ya wanyamapori ili kuvutia watalii
wengi kwa lengo la kuliongezea Taifa mapato.
Jenerali Mstaafu Waitara
ameyasema hayo jana Julai 12, 2025, alipotembelea Banda la Wizara ya Maliasili
na Utalii katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba
yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Jenerali Waitara alisema,
“Ukanda wa Kusini una hazina kubwa ya vivutio vya kipekee ambavyo vinaweza kuwa
kichocheo kikubwa cha uchumi na utalii endapo vitawekewa nguvu ya uwekezaji na
kutangazwa kikamilifu, ni muda muafaka sasa kwa sekta binafsi kushirikiana na
Serikali kupitia TANAPA katika kuibua na kuendeleza maeneo hayo, ili kupanua
wigo wa kitalii na kuongeza pato la Taifa kupitia sekta hiyo.”
“Kama ilivyozoeleka
wawekezaji wengi wa sekta ya utalii wamewekeza sana upande wa Kaskazini katika
mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. Ni wakati sasa wa kugeukia Hifadhi za Kusini
katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe na Katavi ili watalii wetu wagawanyike
kwa ajili ya kupata vionjo na ladha tofauti ya utalii wa kitamaduni kwa
makabila ya wahehe, Wangoni, Wagongwe na makabila mengine ya Kusini, pia waonje
mazingira mengine yenye vivutio tofauti na vilivyopo katika maeneo ya
Kaskazini. Kwa kufanya hivyo tutapunguza msongamano wa watalii eneo moja na
mapato ya utalii kuelekea maeneo ya Kusini pia.”
Vilevile Jenerali Waitara
aliongeza kuwa Hifadhi za kusini kama Ruaha ilishinda tuzo ya kivutio bora cha
kiutamaduni barani Afrika, na Kitulo ikinyakua tuzo ya eneo bora la fungate
Afrika, hivyo sifa hizi na nyingine kedekede zinatarajia kuleta watalii wengi
ndio maana tunawasisitiza kuwekeza upande huo kwani wawekezaji hawatajutia
fedha zao walizowekeza.
Aidha, Waitara alieleza
kuwa zaidi ya watu elfu sita wamepita kutembelea banda la Wizara ya maliasili
na utalii katika maonesho hayo, hatua inayodhihirisha mwitikio chanya wa
wananchi katika kujifunza masuala ya uhifadhi na utalii.
Naye, Kamishna Msaidizi
wa Uhifadhi TANAPA, Neema Mollel, alisema kuwa TANAPA imetumia fursa ya
maonesho hayo kama jukwaa la kutoa elimu
kwa umma, kutangaza vivutio vya utalii pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatika
katika Hifadhi za Taifa.
Maonesho ya 49 ya
Biashara ya Kimataifa Sabasaba yalianza rasmi Juni 28, na yanatarajiwa kufungwa
kesho Julai 13, huku yakibeba kaulimbiu inayosema “Maonesho ya Kibiashara ya
Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania.”
0 Maoni