Waziri wa Maliasili na
Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, ameipongeza Wizara pamoja na taasisi na idara
zake kwa ubunifu mkubwa unaosaidia kuvutia wananchi na watalii wa ndani kutembelea
vivutio vya utalii nchini.
Akizungumza leo Julai 12,
2025, alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya
48 ya Kimataifa ya Biashara (Saba Saba), Dk. Chana alisema banda hilo
limeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wananchi kutokana na huduma na taarifa
mbalimbali zinazotolewa na taasisi na idara zake.
“Nimepokea taarifa kwamba
wananchi wengi wametembelea banda la Wizara, jambo linalothibitisha ubunifu
mkubwa katika kutoa elimu kuhusu uhifadhi na vivutio vyetu,” alisema Dk. Chana.
Aidha, Waziri amewahimiza
wananchi kuendelea kutembelea vivutio vilivyopo nchini, akisisitiza kuwa utalii
wa ndani umekuwa ukikua hususan katika misimu ya sikukuu na matamasha kama haya
ya Saba Saba kutokana na ofa na huduma zinazotolewa.
Dk. Chana alimshukuru
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea
kuboresha miundombinu inayowezesha watalii kufika kwa urahisi kwenye hifadhi na
vivutio vya asili.
“Tunapaswa kuunga mkono
jitihada za Mhe. Rais kupitia filamu za The Royal Tour na Amazing Tanzania,
ambazo zimechangia kwa kiwango kikubwa kutangaza utalii wetu ndani na nje ya
nchi,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri,
filamu hizo zimechangia kuongeza idadi ya watalii, hatua inayosaidia kukuza
kipato cha wananchi na pato la Taifa kwa ujumla.
Aidha, aliwataka wananchi
kuwa mabalozi wazuri kwa kuitangaza Tanzania na kutumia elimu wanayopewa na
wataalamu wa uhifadhi ili kulinda misitu na maeneo yote yaliyohifadhiwa.
“Nawaomba wadau na
wananchi wasibaki tu kwenye maonesho ya Saba Saba, bali pia waendelee
kutembelea hifadhi za misitu na vivutio vingine, mfano hifadhi za misitu ya
asili chini ya usimamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),”
aliongeza.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bi.
Latifa M. Khamis, aliipongeza Wizara na idara zake kwa kuongoza kwa kuwa na
wageni wengi zaidi ya 600,000 waliotembelea banda hilo na kupata elimu ya
uhifadhi na utalii.
Alibainisha kuwa TanTrade
inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo kuimarisha miundombinu na
kuongeza thamani ya bidhaa na huduma zinazotolewa
kupitia maonesho hayo.
0 Maoni