Balozi Batilda asema Tanga ina hifadhi ya lita za ujazo milioni 210 za mafuta

 

UWEKEZAJI mkubwa uliofanywa na Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya nishati, umeuwezesha Mkoa wa Tanga kuwa na hifadhi ya lita za ujazo milioni 210 za mafuta ya petroli na dizeli.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dkt Batilda Burian, amesema hayo leo Julai 15, 2025, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Kikao hicho ni sehemu ya utaratibu wa Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, kuwaalika Wakuu wa Mikoa kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe Rais Dkt Samia.

Mhe Balozi Dkt. Batilda amesema, kiasi hicho cha mafuta kinachohifadhiwa kwenye tenki za mafuta za kampuni ya GBP, kinakidhi matakwa ya kanuni za nishati hiyo na maagizo ya Mhe Rais Dkt. Samia, kusambazwa kwenye mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Amesema usambazi wa mafuta kutokea mkoani Tanga, kunachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za usafirishaji kwa wafanyabiashara, hivyo bei kuwa rafiki kwa watumiaji.

Mhe Balozi Dkt. Batilda amesema hifadhi hiyo ya mafuta, ni sehemu ya fursa nyingi za kiuchumi zilizopo na zinazoendelea kukua mkoani Tanga, tangu Mhe Rais Dkt. Samia kuingia madarakani 2021.

NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Mhe Balozi Dkt Batilda amesema, Tanga inaendelea kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi, taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali.

Kwa mujibu wa Mhe Balozi Dkt. Batilda, hadi sasa taasisi 1,493 za Serikali zenye watumiaji 735,372 wa nishati safi ya kupikia zimetambuliwa.

BOMBA LA MAFUTA GHAFI

Mhe Balozi Dkt. Batilda amesema, Mradi wa Bomba na Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) wenye urefu wa kilomita 205.91 unaohusisha ujenzi wa kituo cha kupokelea, kuhifadhi na kusafirisha mafuta, usimamizi na uendeshaji wa mradi na matenki manne, umekamilika kwa asilimia 53.

Amesema, fidia kwa wakazi waliopisha mkuza wa EACOP mkoani Tanga umefikia asilimia 98.7 ambapo kati ya wananchi 1560 kati ya wanufaika 1580 wameshapokea malipo ya fidia inayofikia Shilingi billion 9.38.

Na. Mashaka Mgeta - Dodoma

Chapisha Maoni

0 Maoni