Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) umeanza kutekeleza ujenzi wa barabara Km 42 kwa
kiwango cha lami kupitia mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya
Pili (DMDP II) katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es
Salaam.
Hayo yameelezwa na
Meneja wa TARURA Wilaya ya Kigamboni, Mhandisi Ismail Mafita ambapo amesema
kuwa mpaka sasa wakandarasi watatu wapo “site” wanaendelea na ujenzi wa
barabara Km 30 huku Km 10.2 zipo katika mchakato wa manunuzi.
“Mpaka kufikia mwisho
wa mwezi Juni mwaka huu zabuni zitatangazwa kwahiyo katika kipindi cha mwezi
mmoja au miwili ijayo hizo Km 10 zitaanza kutekelezwa,” amesema Mhandisi
Mafita.
Amesema kuwa tayari
mradi wa DMDP II umeshaanza kuleta matokeo kwani barabara ambazo zilikuwa na
changamoto zimeshaanza kufanyiwa kazi na wanatarajia mwakani mwezi Februari au
Machi barabara zote Km 42 zitakuwa zimekamilika na kuleta matokeo makubwa
katika manispaa ya kigamboni.
“Jumla ya fedha
zilizotengwa ni shilingi bilioni 100 lakini kwa Km 30 ambazo tayari wakandarasi
wapo “site” zina jumla ya shilingi bilioni 78, kwakweli ni fedha nyingi lakini
pindi mradi utakapokamilika wananchi watanufaika na miundombinu hii.”
Ameeleza kuwa kazi
zitakazofanyika katika mradi wa DMDP II ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha
lami, njia za waenda kwa miguu, vituo vya daladala, taa za barabarani na
mifereji ambapo amewaomba wananchi wawe watulivu katika kipindi cha mpito cha
ujenzi mara baada ya shughuli za ujenzi kukamilika mitaa yote itapendeza na
itakuwa safi na salama.
Mhandisi Mafita
ameongeza kwamba wanaendelea kutekeleza miradi mingine mbalimbali katika wilaya
hiyo ambayo imepata bajeti ya bilioni 5 kwa ujenzi wa barabara ya Kivukoni
Primary School na Rombo Bar kwa kiwango cha lami Km 0.62, pia mkandarasi yupo
kazini anakamilisha mita 500 katika barabara kuu inayoelekea daraja la Mwl.
Nyerere ambapo zikikamilika zitasaidia wakazi wa Kigamboni wanaoelekea maeneo
ya Kivukoni au darajani kutumia barabara bila changamoto yoyote.
Naye, mkazi wa mtaa
wa Salanga Kigamboni, Bw. Stephano James amesema awali walikuwa na changamoto
ya barabara, mvua zikinyesha maji yakijaa pikipiki zao zilikuwa zinaharibika
lakini sasa wanafanya kazi zao bila shida na wanaiomba serikali iendelee
kuwaboreshea miundombinu ili kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.
Bw. Ally Yusuph mkazi
wa kata ya Vijibweni Kigamboni, amesema kuwa adha kubwa waliyokuwa wanaipata ni
vumbi, madimbwi na matope lakini barabara ikiwekwa lami watafurahi sana na
wanaomba mkandarasi asimamiwe ili kazi ikamilike kwa wakati.
Farid Yusuph mkazi wa
mtaa wa feri Kigamboni ameishukuru serikali kwa kuwaboreshea miundombinu na
ameomba waongezewe alama za barabarani na matuta na pia ameomba wananchi
wenzake wailinde miundombinu hiyo kwa kuwa wastaarabu na kutotupa takataka
kwenye mifereji.
0 Maoni