Bodi ya Ushauri ya
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeitaka taasisi hiyo kuandaa siku
maalum ya kitaifa kwa ajili ya kutangaza fursa za utalii na uwekezaji katika
vivutio vya utalii kwenye Hifadhi za Misitu, huku ikiweka msisitizo kwenye
misitu yenye vivutio vya kipekee kama Ziwa Duluti kuwa kitovu cha utalii wa
ndani na chanzo cha mapato kwa jamii na serikali.
Kauli hiyo ilitolewa
Juni 25, 2025 na Mjumbe wa Bodi hiyo, Mhandisi Enock Emmanuel Nyanda, wakati wa
ziara ya siku ya pili ya Bodi ya TFS katika Kanda ya Kaskazini, iliyofanyika
kwenye eneo la hifadhi ya Ziwa Duluti, wilayani Arumeru mkoani Arusha.
“Tanzania imejaa
vivutio vya kipekee vilivyomo ndani ya Hifadhi za misitu, lakini havijatumiwa
kikamilifu. Tuna vivutio kama Ziwa Ngosi lililoko Uporoto, Mbeya – la pili kwa
ukubwa barani Afrika kwa maziwa ya asili ya milipuko ya volkano – lakini hakuna
mwekezaji hata mmoja. TFS inapaswa kuandaa ‘Siku ya Utalii wa Misitu’ kutangaza
hazina hii,” alisema Nyanda, ambaye pia Mkurugenzi Msaidi Idara ya Uratibu wa
Sekta Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Kwa mujibu wa Nyanda,
uwekezaji uliofanyika Ziwa Duluti kupitia kampuni ya SS Camps unaoongozwa na
Mkurugenzi Mtendaji wake, Mwanadada Suzan Minja, unapaswa kuigwa na
kuhamasishwa kwenye misitu mingine nchini ili kufungua fursa za kiuchumi, ajira
na utalii wa ndani.
Awali, Mhifadhi
anayesimamia Hifadhi ya Ziwa Duluti, Peter Myonga, aliwapokea wajumbe wa Bodi
na kuwaeleza kuwa eneo la Ziwa Duluti linaendelea kuboreshwa kwa kuimarisha
miundombinu ya utalii ikiwemo ujenzi wa vyumba vya malazi, mgahawa na njia za
kutembelea maeneo ya mapangoni ambako hufanyika ibada za jadi.
“Vyumba 10 vya kulala
wageni viko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Pia tunaendeleza eneo la mgahawa
litakalosaidia wageni kupata huduma muhimu wakati wa matembezi,” alisema
Myonga.
Mwekezaji katika eneo
hilo, Bi. Suzan Minja, alisema uwekezaji unaofanyika unalenga kuongeza ajira
kwa vijana wa eneo hilo, kukuza uchumi wa jamii na kusaidia uhifadhi wa
mazingira kwa kuzingatia matumizi rafiki ya rasilimali.
“Tulipokuta eneo hili
halikuwa na miti, lakini tumejenga kwa kuzingatia mipaka ya hifadhi na
kuhifadhi miti yote iliyokuwepo. Hii ni njia endelevu ya kuleta maendeleo
pasipo kuharibu mazingira,” alisema Bi. Minja.
Nyanda pia
alisisitiza umuhimu wa TFS kushirikiana na taasisi za elimu ya juu, sekta
binafsi na wadau wa mazingira kuandaa maonesho ya kitaifa yatakayojulikana kama
‘Siku ya Misitu Tanzania’ ili kuonesha bidhaa, huduma na fursa zinazopatikana
katika misitu ya asili na mashamba ya miti.
“TFS si taasisi ya
kukusanya tu mapato, bali ni mhimili wa uhifadhi, uendelezaji wa mazingira na
uchumi wa kijani. Misitu yetu inaweza kuwa mazao ya utalii kama ilivyo kwa
wanyamapori,” alieleza.
Ziara hiyo ya Bodi ya
Ushauri ya TFS inalenga kutathmini utekelezaji wa miradi ya maendeleo, usimamizi
wa misitu, ukusanyaji wa mapato na ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi
katika kanda mbalimbali nchini.
0 Maoni