Shamba la Miti Meru-Usa lavutia uwekezaji, lavunja rekodi ya mapato na idadi ya watalii

 

Shamba la Miti la Meru-Usa, linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), limeibuka kuwa mfano wa mafanikio katika uwekezaji na utendaji baada ya kuvuka malengo ya uzalishaji, mapato, na idadi ya watalii kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Katika taarifa yake kwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya TFS, iliyotolewa Juni 25, 2025, wakati wa ziara ya siku mbili ya bodi hiyo (Juni 24–25), Mhifadhi Mkuu wa Shamba hilo, Ali D. Maggid, alieleza kuwa mapato ya shamba hilo yamefikia Shilingi bilioni 4.4 dhidi ya lengo la Shilingi bilioni 3.5, ikiwa ni utekelezaji wa asilimia 122.

“Kupitia mkakati madhubuti wa ukusanyaji mapato na uvunaji wa magogo ya thamani kubwa, tumevuka makadirio ya mapato kwa zaidi ya Shilingi milioni 900. Tunajivunia kuwa sehemu ya mabadiliko chanya ya uchumi wa sekta ya misitu nchini,” alisema Maggid.

Aidha, idadi ya watalii wa ndani na nje imeongezeka kwa kasi, kutoka 7,300 mwaka 2021/2022 hadi 32,000 mwaka 2024/2025, na kuchangia zaidi ya Shilingi milioni 236 katika mapato ya utalii wa ndani pekee.

“Eneo la Napulu Waterfalls lililopo ndani ya shamba hili limekuwa kivutio kikubwa cha utalii wa ikolojia, hasa kutokana na ukaribu wake na Jiji la Arusha. Hii imerahisisha kwa wageni kuutembelea hata kwa muda mfupi wa jioni,” aliongeza Maggid.

Katika eneo la uzalishaji wa miche, shamba hilo limesambaza miche 1,000,385 dhidi ya lengo la miche 1,000,000, huku mbegu bora za miti zikitolewa kwa taasisi mbalimbali na wananchi. Hata hivyo, changamoto ya matumizi yasiyo rasmi ya miche hiyo imebainika, baadhi ya wananchi wakihusishwa na kuiuza kinyume na makusudio ya upandaji.

Shamba hilo pia limeanza ujenzi wa miundombinu muhimu ya utalii, ikiwemo ofisi, nyumba ya walinzi, na jengo la huduma kwa gharama ya Shilingi milioni 171.6, ambapo kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo Julai 15, 2025.

Katika mchango wake kwa jamii, Shamba la Meru-Usa limekuwa likisaidia vifaa vya ujenzi kwa shule, zahanati, na ofisi za vijiji. Aidha, wananchi wa vijiji 32 vinavyozunguka shamba hilo hupewa fursa ya kulima katika maeneo yaliyoandaliwa kwa ajili ya upandaji mpya wa miti, hatua inayosaidia kuongeza uhakika wa chakula.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya TFS, Enock Emmanuel Nyanda, Mkurugenzi Msaidi Idara ya Uratibu wa Sekta Ofisi ya Rais TAMISEMI, alisisitiza umuhimu wa TFS kutumia takwimu chanya za utendaji kama nyenzo ya kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi kupitia majukwaa ya kitaifa kama Sabasaba na Nane Nane.

“TFS inapaswa kuwa kinara wa kuonesha fursa za uwekezaji katika rasilimali za misitu, hasa maeneo kama Meru-Usa yenye jiografia rafiki kwa utalii wa muda mfupi. Hili ni eneo la kimkakati linalopaswa kuendelezwa zaidi,” alisema Nyanda.



Chapisha Maoni

0 Maoni