Wachimbaji wadogo kutoka migodi ya shaba iliyopo katika Mkoa wa Dodoma wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu usalama mahali pa kazi, afya, utunzaji wa mazingira na usimamizi wa shughuli za uchimbaji.
Mafunzo hayo ni
sehemu ya jitihada za kuimarisha uchimbaji salama na endelevu nchini.
Mafunzo hayo
yamewahusisha wachimbaji kutoka Mgodi wa Shengde uliopo Nala, Mgodi wa Hussein
Pilly uliopo Tambi (Wilaya ya Mpwapwa) na Mgodi wa Canada uliopo Chamkoroma
(Wilaya ya Kongwa) ambapo yamewezeshwa na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa
Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Tume ya Madini.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhandisi Chacha Megewa kutoka Tume ya Madini ameeleza
kuwa ni muhimu kwa wachimbaji kufanya kazi katika mazingira salama kwa kutumia
vifaa kinga kama kofia ngumu, reflekta, buti, gloves na barakoa (maski).
"Ulipuaji wa
baruti ni mojawapo ya shughuli hatarishi migodini, hii ni kazi ya kitaalam na
lazima ifanywe na mtu mwenye cheti maalum,
ni muhimu kuhakikisha vilipuzi vyote vimelipuka kikamilifu kabla ya
kuruhusu watu kuingia mgodini tena," amesisitiza Mhandisi Megewa.
Kwa upande wake,
Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini, Fahad Mkuu, amekumbusha kuwa usalama
ni jukumu la pamoja na si la mtu mmoja.
Amesisitiza umuhimu wa wachimbaji kujenga
utamaduni wa kulinda afya zao na kuheshimu kanuni za kazi migodini.
"Mazingira ya
mgodi ni hatarishi. Kutovaa vifaa kinga ni kuhatarisha maisha yako, ni jukumu letu sote kulinda afya zetu na
kuhifadhi mazingira," amesema.
Fahad ameongeza kuwa
hatua za kurekebisha mazingira baada ya uchimbaji ikiwemo kufukia mashimo na
kupanda miti ni muhimu kwa usalama wa jamii, hasa watoto na mifugo.
Wakati wa
majadiliano, baadhi ya wachimbaji wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo na
kuomba kupewa msaada wa vifaa vya kujikinga ili kusaidia kulinda afya ya uzazi
na kupunguza maambukizi ya VVU katika maeneo ya migodi.
Mafunzo haya ni
sehemu ya mikakati ya UNDP ya kuimarisha mchango wa Sekta ya Madini nchini kwa
kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinakuwa salama, zenye tija na zinazozingatia
masuala ya afya na mazingira.
Kwa mujibu wa
waandaaji, mafunzo kama haya yataendelea kutolewa katika mikoa mingine ili
kusaidia kuwawezesha wachimbaji wadogo kuendana na viwango vya kitaifa na
kimataifa vya uchimbaji bora na salama.
0 Maoni