WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa nguzo ya kuimarisha mshikamano na umoja wa kitaifa na kufanikisha maendeleo katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Amesema kuwa katika
kipindi cha uongozi wake, Rais Dkt. Samia ameweza kusimama imara katika
kuendeleza miradi ya kimkakati na huduma za jamii, kusimamia demokrasia,
kujenga uchumi na kuimarisha diplomasia.
Amesema hayo leo
(Alhamisi, Juni 26, 2025) wakati alipotoa hoja ya kukamilisha shughuli za Bunge
la 12, Bungeni jijini Dodoma.
“sina shaka nyote
mtakubaliana nami kuwa hulka yake na ustahimilivu wake umekuwa faraja kwetu
sisi wasaidizi wake, watumishi wote wa umma na Watanzania wote kwa ujumla.
Isitoshe, Mheshimiwa Rais wakati wote amekuwa nguzo ya kuimarisha mshikamano na
umoja wa kitaifa.”
Amesema Mheshimiwa
Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa Mwalimu wa subira, kielelezo cha ujasiri,
ustahimilivu na alama ya matumaini kwa kizazi hiki. “Ni kiongozi aliyetoa mfano
wa kuwa mwanamke anaweza kuongoza hata kwenye nafasi ya Kitaifa.”
Kadhalika, Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa kutokana na uongozi dhabiti wa Rais Dkt. Samia, taasisi
mbalimbali za kitaifa na kimataifa zimetambua mchango na maono yake katika kusimamia
shughuli za kimaendeleo nchini na kuitangaza Tanzania nje ya nchi.
Mheshimiwa Majaliwa
ametaja tuzo alizopokea kimataifa kuwa ni Global Gates Goalkeepers, Tuzo ya
Babacar Ndiaye kwa mwaka 2022, Tuzo ya Uongozi wa Kimageuzi Afrika, Tuzo ya
Heshima ya Pyne Africa Awards 2022 na Tuzo ya Muongoza Watalii Bora.
Tuzo nyingine
alizopata kitaifa ni Tuzo Maalum ya Heshima ya kutambua mchango wake katika
kulitumikia Taifa na kuwaletea wananchi maendeleo iliyotolewa na Bunge, Tuzo
Maalum ya kutambua dhamira yake thabiti ya kujenga Taifa linalostahimili
Mabadiliko ya Tabianchi.
“Tuzo nyingine
alizopata kitaifa ni kutambua mchango wake katika kuendeleza sekta ya kilimo
nchini, tuzo Maalumu ya kutambua mchango, maono na uongozi wake katika kuifanya
elimu kama nguzo kuu ya maendeleo ya nchi na tuzo ya Ubinadamu ya kutambua na
kuheshimu mchango wake katika masuala mbalimbali yanayogusa jamii ya Watanzania.”
Ameongeza kuwa
jitihada za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika nyanja mbalimbali zimetoa
msukumo kwa wanazuoni katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya Tanzania kumtunuku
Shahada ya Juu ya Udaktari wa Heshima.
Ametaja vyuo hivyo
kuwa ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA),
Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru kilichopo New Delhi nchini India, Chuo Kikuu
cha Ankara cha nchini Uturuki na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Jamhuri ya
Korea.
Katika hatua nyingine
Mheshimiwa Majaliwa amewapongeza watendaji wote wa Serikali kwa kutekeleza kwa
vitendo maono ya Rais Dkt. Samia. “Leo tunajivunia mafanikio makubwa katika
utendaji wa Serikali kwa kila sekta hapa nchini. Mafanikio hayo yanatokana na
kujitoa kwao katika kuhakikisha mikakati na maono vinatekelezwa kama
ilivyokusudiwa”.
0 Maoni