Bunge limeridhia ombi
la Serikali la kumega sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa lengo la
kutatua migogoro ya mipaka na kuwezesha shughuli za maendeleo kuendelea katika
mazingira rafiki kwa jamii na uhifadhi.
Waziri wa Maliasili
na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana, akiwasilisha azimio hilo
bungeni, amesema kuwa Serikali imeamua kumega eneo lenye ukubwa wa kilomita za
mraba 1,617 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kulirejesha katika Pori la
Akiba Selous.
Amesema hatua hiyo
imepunguza ukubwa wa hifadhi hiyo kutoka kilomita za mraba 30,893 hadi kufikia
kilomita za mraba 29,276.
Akifafanua zaidi,
Mhe. Chana amesema hatua hiyo inalenga kuondoa migogoro ya muda mrefu ya mipaka
baina ya hifadhi hiyo, vijiji vinavyoizunguka, Pori la Akiba Selous na Jumuiya
za Hifadhi za Wanyamapori za Mbarang’andu, Juhiwangumwa, Iluma, Jukumu, Magingo
na Nalika.
“Kwa kufanya hivyo,
tunaimarisha usalama wa maeneo yaliyohifadhiwa, tunajenga mahusiano bora kati
ya wananchi na hifadhi, na kuondoa migogoro iliyodumu kwa muda mrefu,” amesema
Mhe. Chana.
Aidha, Waziri huyo
ameeleza kuwa marekebisho hayo ya mpaka yanalenga kulinda mfumo ikolojia muhimu
unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Pori la Akiba Selous, sambamba na
kuhakikisha mtiririko endelevu wa maji katika Mto Rufiji, ambao ni chanzo kikuu
cha uzalishaji umeme kupitia Mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP).
Mhe. Chana
amebainisha kuwa hatua hiyo itaongeza tija kwa Taifa kwa kuimarisha shughuli za
utalii, uwindaji wa kitalii katika Pori la Akiba Selous na maeneo
yanayozunguka, na hivyo kuchangia mapato ya ndani kupitia sekta ya utalii.
“Kwa sasa, tunaelekea
katika uboreshaji wa uhifadhi wa maliasili kwa ujumla wake – wanyamapori,
mimea, mazalia ya viumbe wa majini na pia kuongeza upatikanaji wa maji kwa
matumizi ya wakulima, wafugaji na wavuvi,” ameongeza.
Na. Anangisye Mwateba-
Dodoma
0 Maoni