Mwanasoka Gavi atua nchini avinjari Hifadhi ya Serengeti

 

Nyota wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Pablo Gavi, amejiunga na orodha ya wachezaji nyota wa kimataifa wanaochagua Tanzania kama sehemu ya mapumziko yao.

Kiungo huyo mahiri yupo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pamoja na mpenzi wake, Ana Pelayo, akifurahia mandhari na vivutio vya kipekee vya nchi.

Ujio wa Gavi unakuja siku chache tu baada ya wachezaji wengine watatu wa soka kutoka Hispania kutua nchini kwa mapumziko. Nyota hao ni pamoja na David Raya wa Arsenal, David De Gea aliyewahi kung’ara Manchester United, na kiungo wa Barcelona, Pedri.

Hii inaongeza idadi ya mastaa wa soka wanaotembelea Tanzania msimu huu wa kiangazi, hali inayoendelea kuiweka nchi kwenye ramani ya kimataifa kupitia utalii.

Mbali na wachezaji hao wa Hispania, Tanzania pia imepokea nyota wengine wawili maarufu duniani; mshambuliaji wa zamani wa Sweden, Barcelona na AC Milan, Zlatan Ibrahimovic, pamoja na Arnaut Danjuma, mshambuliaji wa Girona na timu ya taifa ya Uholanzi.

Tanzania imeendelea kuvutia wageni maarufu kwa vivutio vyake vya kipekee kama Hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro na Visiwa vya Zanzibar, huku mastaa hao wakichangia kuiweka nchi kwenye jicho la dunia kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya kimataifa.




Chapisha Maoni

0 Maoni