Sekta ya Madini nchini Tanzania inaendelea kushamiri kwa kasi,
ikifungua milango ya ajira, uwekezaji na maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Serikali kupitia Tume ya Madini imeendelea kuweka mazingira
wezeshi kwa kuhakikisha usimamizi madhubuti, uwazi, na ushirikishwaji wa wadau
wote katika mnyororo mzima wa shughuli za madini. Haya yamekuwa ni matokeo ya
maboresho ya sera, sheria, pamoja na mifumo ya kidijitali inayotumika katika
kusimamia sekta hiyo.
Akizungumza leo Juni 21, 2025 katika Maadhimisho ya Wiki ya
Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma,
Afisa Ukaguzi Migodi kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wa Tume
ya Madini, Bw. Ashen Mwambage, amesema kuwa Watanzania wengi wanapaswa
kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa kupitia Sekta ya Madini.
Ameeleza kuwa katika mikoa mbalimbali kama Geita, Shinyanga, Mara
na Mbeya, wananchi wamehamasika kushiriki katika shughuli za uchimbaji mdogo wa
madini, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato cha familia na
kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha fursa hizi zinamfikia
kila Mtanzania. Kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa katika mikoa
mbalimbali, sasa bei ya madini iko wazi, mapato ya Serikali yanaongezeka na
wachimbaji wananufaika kwa haki,” amesema Bw. Mwambage.
Kwa upande wa teknolojia, amesema Serikali imekuwa mstari wa mbele
kusukuma matumizi ya mbinu za kisasa katika utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji
wa madini ili kuongeza ufanisi, kupunguza athari za mazingira na kuhakikisha
usalama kwa wachimbaji wadogo. Hii imeenda sambamba na utoaji wa mafunzo ya
mara kwa mara kwa wachimbaji hao.
“Hatupaswi kuuza madini ghafi, bali kuongeza thamani hapa hapa
nchini. Uongezaji thamani madini umefungua fursa nyingi za ajira, ujasiriamali,
na kuinua Pato la Taifa,” ameongeza.
Aidha, Bw. Mwambage amesema kuwa mchango wa Sekta ya Madini
umeendelea kuibua fursa kwenye sekta nyingine kama uchukuzi, huduma za malazi,
usafirishaji wa mizigo, huduma za kifedha na bima, hali inayoonesha namna sekta
hiyo inavyobeba uchumi wa nchi kwa mapana yake.
Tume ya Madini inatoa wito kwa Watanzania wote, hususan vijana,
kuchangamkia fursa zilizopo kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa ili
waweze kunufaika na rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kizazi cha
sasa na kijacho.
0 Maoni