Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imeipongeza TANAPA kwa
ushirikiano mkubwa unaoendelea kuoneshwa katika kuendeleza sekta ya utalii na
kuhifadhi urithi wa Taifa, kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Utalii na
Uwekezaji yanayofanyika katika viwanja vya Dimani Fumba, Zanzibar.
Akizungumza jana Juni
20, 2025 Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga,
alisema TANAPA kupitia Ofisi Kiunganishi ya Zanzibar imekuwa mfano bora wa
taasisi inayoshirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii, na
kuwa cheti cha heshima walichotunukiwa ni alama ya kutambua mchango wao katika
kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo.
Awali, akiongea kwa
niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Fredrick
Malisa anayeshughulikia Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Kanda ya Mashariki,
alisema shirika linaendelea kujipambanua kama mdau mkuu katika kukuza utalii
endelevu na kuvutia uwekezaji katika Hifadhi 21 za Taifa. Alisisitiza kuwa
maonesho haya yamekuwa jukwaa muhimu kwa TANAPA kuwasiliana moja kwa moja na
wawekezaji na kuwakaribisha kushirikiana katika katika kutambua fursa za utalii
na uwekezaji.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Ofisi Kiunganishi ya TANAPA Visiwani
Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Halima Kiwango, alieleza
kuwa TANAPA imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kushirikiana na Serikali na
wadau kwa kutoa taarifa ya vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi za
Taifa, fursa za uwekezaji na huduma kwa watalii sanjari na mazao ya utalii.
Naye mdau wa utalii
kutoka Zanzibar, Sabra Saleh, alisema ushiriki wa TANAPA katika maonesho hayo
umeleta hamasa kubwa kwa vijana na wadau wa ndani kuingia kwenye sekta ya
utalii. Alisema Shirika linaonesha mwelekeo mzuri wa utalii wa asili unaojengwa
katika misingi ya ushirikiano na maendeleo kwa jamii.
Kwa ujumla, ushiriki
wa TANAPA katika maonesho haya ni kielelezo cha dhamira ya Shirika hilo kuendelea
kushirikiana na wadau wote wa maendeleo ndani na nje ya nchi, katika kulinda
urithi wa Taifa, kukuza utalii endelevu na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye
maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia uhifadhi na Utalii.
0 Maoni