Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na
Waziri wa Nishati wa Urusi, Mhe. Sergey Tsivilev kuhusu kuimarisha
ushirikiano katika sekta ya nishati na
maeneo mengine muhimu ikiwemo teknolojia na uwekezaji.
Mazungumzo hayo kati
ya Dkt. Biteko na Mhe. Tsivilev yamefanyika kando ya Jukwaa la Kimataifa la Uchumi St. Petersburg nchini
Urusi.
Kupitia mkutano huo
Dkt. Biteko amesema kiwango cha uwekezaji
nchini kutoka Urusi kinafikia
dola za Kimarekani milioni 424 kupitia miradi 44 inayoajiri watu zaidi
ya 3,000 huku akielezea fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya nishati.
"Tanzania ina
asilimia 61.7 ya nishati kutoka vyanzo vinavyoweza kurejeshwa na fursa za
uwekezaji zenye thamani ya dola bilioni 4 katika sekta ya nishati,"
amesema Dkt. Biteko.
Ametaja jitihada za
Serikali katika kuleta mageuzi kwenye sekta ya nishati sambamba na kushirikisha
sekta binafsi kwenye utekelezaji wa miradi ya pamoja na kuhamasisha matumizi ya
nishati safi ya kupikia akitolea mfano Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za
Afrika uliofanyika Dar es Salaam mwezi Januari 2025 uliolenga kutoa umeme kwa
waafrika milioni 600 ambao hawana umeme.
Pia, Dkt. Biteko
amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Urusi kuongeza uwekezaji nchini hususan
katika nishati safi ya kupikia ambapo ameelezea uwepo wa fursa za uwekezaji wa
sekta binafsi za uzalishaji umeme wa
kujitegemea na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi.
Fauka ya hayo, Dkt.
Biteko amefurahishwa na uhusiano wa kidiplomasia wa takribani miaka 64 kati ya
Tanzania na Urusi na kusema kuwa uhusiano huo unalenga kunufaisha wananchi wa
nchi hizo.
Kwa upande wake,
Waziri wa Nishati wa Urusi, Mhe. Sergey Tsivilev amezungumzia umuhimu wa
nishati katika maendeleo ya kiuchumi hususan katika masuala ya usalama wa
nishati, upatikanaji, bei nafuu, na ufanisi.
Mhe. Tsivilev amesema
kuwa Urusi ipo tayari kusaidia teknolojia na kujengea uwezo wataalamu wa Afrika
ikiwemo Tanzania ili kuhakikisha uhuru wa teknolojia unakuwepo.
"Urusi ina mkakati
wa haki katika ushirikiano na malengo ya kuendeleza mifumo ya nchi kwa
washirika wa muda mrefu," amesema
Mhe. Tsivilev.
Amezungumzia maeneo
mengine ambayo Urusi imeahidi kuisaidia Tanzania ni pamoja na afya, usalama wa
mtandao na ulinzi wa miundombinu muhimu.
Naye, Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya INTER RAO Export, ambayo ni moja ya Kampuni kubwa zaidi
ya nishati duniani, Bw. Maxim Sergeev licha ya
kuonesha nia ya kuwekeza nchini amesema
kuwa Kampuni hiyo ina uwezo wa kutengeneza vifaa mbalimbali ikiwemo mashine
umba na jenereta pia ina mikataba ya kila mwaka inayofikia dola bilioni 8.
Aidha, mazungumzo
hayo kati ya Dkt. Biteko na Tsivilev yamehudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania
Moscow, Mhe. Frederick Kibuta,
Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi John Ulanga na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo
ya Petroli, Mhandisi Marwa Petro.
Kando ya
mazungumzo hayo naye Mkurugenzi Mtendaji
wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange amefanya mazungumzo na
Kampuni ya Rosatom na Unigreen kuhusu ushirikiano wa uzalishaji wa umeme
unaotokana na urani pamoja na jua ambapo Unigreen inaendelea na taratibu za
uwekezaji nchini.
Na. Ofisi ya Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni