Bwana Rémy Rioux,
Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AfD), akizungumza
mbele ya wajumbe wa Mkutano wa siku mbili wa Bodi ya Taasisi ya Ubia wa Elimu
Duniani (Global Partnership for Education – GPE) unaofanyika mjini Paris,
Ufaransa, leo tarehe 3 Juni 2025, chini ya uenyekiti wa Rais Mstaafu wa
Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Mkutano huo
umewakutanisha wajumbe zaidi ya 40 wanaowakilisha makundi mbalimbali ya ubia
huo, wakiwemo wawakilishi kutoka nchi saba tajiri zaidi duniani (G7), pamoja na
nchi washirika kutoka kanda zinazoendelea kiuchumi, hasa Afrika na Asia.
Vilevile, mashirika mbalimbali ya kimataifa yanashiriki katika mjadala huo
muhimu wa elimu.
Katika kikao hicho,
Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Ali Jabir Mwadini, alitumia
nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Ufaransa kwa ushirikiano thabiti uliopo kati
ya Tanzania na Ufaransa. Alisisitiza utayari wa Tanzania kuendeleza na kukuza
zaidi mahusiano hayo ya kidiplomasia na ya kimkakati kwa manufaa ya pande zote
mbili, hasa katika sekta ya elimu.
Mkutano huo wa GPE
unalenga kujadili namna taasisi hiyo inaweza kuhimili na kukabiliana na
changamoto za sasa duniani, ikiwemo mabadiliko ya sera za kimataifa, huku
ukibeba matumaini ya kuboresha usawa na ubora wa elimu katika nchi
zinazoendelea.
Katika picha ya pamoja, kutoka kushoto ni: Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Ali Jabir Mwadini; Bi. Christine Hogan, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Global Partnership for Education (GPE); Bw. Rémy Rioux, Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AfD); Rais Mstaafu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Bodi ya GPE, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete; Bi. Eléonore Caroit, Mbunge na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ufaransa; na Bi. Laura Frigenti, Afisa Mtendaji Mkuu wa GPE.
0 Maoni