Waziri wa Maliasili
na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amewavisha cheo manaibu kamishna wawili
na kushuhudia uvishwaji vyeo kwa makamishna wasaidizi waandamizi watano
waliovishwa vyeo na mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi NCAA Jenerali Venance
Mabeyo (Mstaafu).
Waliovishwa Cheo na
Mhe. Waziri ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Joas John Makwati
aliyepandishwa cheo kuwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Uhifadhi,
utalii na Maendeleo ya Jamii na Naibu Kamishna wa Uhifadhi Aidan Paul Makalla
anayesimamia Huduma za Shirika NCAA.
Kwa upande wa
makamishna waliovishwa vyeo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NCAA Jenerali
Venance Mabeyo (mstaafu) ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi
anayesimamia idara ya Mipango na uwekezaji, Gasper Stanley Lyimo, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Paul Geofrey Shaidi anayesimamia Kitengo cha
huduma za Sheria, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Charles Marwa Wangwe
anayesimamia Idara ya Uhasibu na fedha.
Wengine ni Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwin Felician Kashaga anayesimamia Kitengo
cha Ukaguzi wa Ndani, na Afisa Uhifadhi Mkuu Daraja la kwanza Mariam Kobelo
anayesimamia idara ya Huduma za Utalii na masoko aliyepandishwa cheo kuwa
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi.
Baada ya kuwavishwa
vyeo hivyo waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb)
amewaelekeza maafisa hao kufanya kazi kwa bidiii na weledi mkubwa katika
kutekeleza majukumu yao kwa kuwa cheo ni dhamana na kinakuja na majukumu.
“Nimatumaini yangu
kuwa viongozi wote mliovaa vyeo leo mtakuwa chachu ya kufanya kazi kwa kujituma
na kuonesha mfano wa kuigwa kwa Maafisa na Askari mnaowaongoza, juhudi zenu
ndiyo zitakazochangia kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro na kuendelea kuwa
kivutio kwa wageni wanaotembelea” ameongeza Balozi Chana.
Kamishna wa Uhifadhi
NCAA Abdul-Razak Badru ameeleza kuwa kwa sasa watumishi wote wa NCAA
wameshapatiwa mafunzo ya kijeshi kutoka mfumo wa awali wa kiraia na kuwa
mamlaka hiyo itahakikisha inatumia rasilimali ya watumishi waliopo kuongeza
nguvu ya kuhifadhi, kulinda, kuendeleza jamii na kuboresha miundombinu ya
utalii.
Mwenyekiti wa bodi ya
NCAA Jenerali, Venance Mabeyo (mstaafu) ameeleza kuwa mafanikio ya Ngorongoro
yanategemea uadilifu na uwezo wa viongozi wake na kuwaasa viongozi waliovishwa
vyeo kubeba matumaini mapya katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi, utalii
na maendeleo ya jamii.
Mabeyo amempongeza
Waziri wa Maliasili na Utalii, Serikali kwa ujumla na wadau wa utalii kwa
kuiunga mkono Ngorongoro na hatimae kutangazwa kama Kivutio Bora cha Utalii
Barani Afrika kwa mwaka 2025.
Na. Kassim Nyaki -
NCAA Arusha
0 Maoni