Zahara Michuzi, mmoja
wa watumishi wa umma waliopitia majukumu makubwa serikalini kwa miaka kadhaa,
amejiunga rasmi katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Viti Maalum kupitia Umoja
wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Tabora.
Katika tukio
lililosubiriwa kwa bashasha na matumaini makubwa, Zahara alipokea rasmi fomu ya
kugombea kutoka kwa Katibu wa UWT wa Mkoa, Bi. Rhoda Sanga. Tukio hilo limezua
msisimko miongoni mwa wanachama wa UWT, huku wengi wakimtaja Zahara kama
mwanamke shupavu na mchapakazi mwenye historia isiyo na doa katika utumishi wa
umma.
Zahara, ambaye
amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji (DED) katika Halmashauri tatu tofauti — Meatu
(Simiyu), Ifakara (Morogoro), na Geita (Geita Mjini) — anajivunia rekodi ya
uongozi ulioleta mabadiliko halisi katika maeneo aliyohudumu. Kabla ya
kupandishwa cheo kuwa DED, aliwahi pia kuwa Katibu Tawala wa Wilaya (DAS)
katika Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, nafasi aliyoitumikia kwa weledi na
kujenga imani kwa viongozi na wananchi.
Kwa kuingia kwake
kwenye siasa, hasa katika nafasi ya uwakilishi wa wanawake kupitia UWT, Zahara
analeta pamoja uzoefu wa kiutawala, usimamizi wa miradi ya maendeleo, na uelewa
wa changamoto halisi zinazowakabili wanawake na jamii kwa ujumla katika mkoa wa
Tabora na Tanzania nzima.
Wadadisi wa siasa
wanaona uamuzi wa Zahara kama hatua ya kuhamasisha wanawake waliobobea katika
sekta ya umma kushiriki moja kwa moja katika uundaji wa sera, hasa zile zinazolenga
ustawi wa wanawake, vijana, na makundi maalum.
0 Maoni