Washiriki watakaojisajili na kushiriki mbio za Fun Run katika Bonanza la Mac D 2025, litakalofanyika Jumamosi tarehe 07/6/2025 kuanzia asubuhi saa 12:00 alfajiri katika viwanja vya Chuo cha Taifa cha Jeshi (NDC), Jijini Dar es Salaam watapatiwa fulana (t-shirt) bure pamoja na namba ya ushiriki.
Mratibu wa Bonanza hilo Denzel Rweyunga, amesema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa EB Twenty Five, na kuongeza kuwa pia washiriki wa mbio hizo za kujifurahisha na kuweka miili sawa kiafya hawatalipia chochote ili kushiriki.
“Katika mwaka huu tumeongeza mbio za kujifurahisha ili kuweka miili yetu katika hali nzuri ya kiafya ambapo hakuna mshindi wala zawadi yeyote itakayotolewa, bali washiriki wote watapatiwa fulana bure na namba za kukimbilia,” alisema Denzel.
Amesema kuwa mbali na mbio hio za saa kumi jioni Mac D FC watashuka dimbani kucheza mchezo wa mpira wa miguu dhidi ya IPP Media, na kuongeza kuwa mwaka huu kutakuwa na Kombe zuri kubwa ambalo mshindi wa mchezo huo ataondoka nalo ambapo mchezo huu utatangazwa moja kwa moja na kituo cha Radio One.
Bonanza la Mac D pamoja na mbio za kujifurahisha (Fun Run) 2025 limedhaminiwa na Bodi ya Utalii Tanzania ( TTB ), Isumba Trans Limited ( ITL ), Kilimanjaro Water, EB Twenty Five, Zakys Bay na Pwani Inland Clearance Deport Ltd (PICD).
0 Maoni