Shirika la Hifadhi za
Taifa Tanzania (TANAPA) limefanikiwa kuendesha mafunzo muhimu ya Usimamizi wa
Viatarishi kwa Wakuu wa Kanda, Wasimamizi wa Ofisi Viunganishi, Maafisa wa
Hifadhi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Mafunzo hayo, yaliyofanyika katika ofisi ya Kiunganishi ya
TANAPA, Dodoma kuanzia Mei 5 hadi 9, 2025, yamelenga kuimarisha ufanisi katika
usimamizi wa viatarishi kwa kutoa ujuzi na mbinu bora za kutambua, kudhibiti,
na kuripoti viatarishi katika ngazi zote za Shirika.
Akizungumza katika katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo haya
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwell Meng’ataki ambaye pia ni Mkuu
wa Kanda ya Kusini alieleza kuwa Semina hii elekezi inalenga kuimarisha ujuzi,
uelewa wa pamoja na mbinu bora za kusimamia vihatarishi jambo ambalo ni msingi
wa Utawala Bora na uwajibikaji wa TANAPA.
“Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za TANAPA, katika
kuhakikisha kuwa utawala bora na uwajibikaji unazingatiwa katika usimamizi wa
Hifadhi za Taifa, hivyo kuimarisha Uhifadhi na Utalii endelevu nchini ni
matarajio yangu kuwa tukirejea katika maeneo yetu ya kazi tutakuwa na nguvu
mpya ya kuhakikisha viatarishi vinatambuliwa, mikakati ya kuvithibiti
inatekelezwa ipasavyo, na taarifa sahihi zinaandaliwa kwa wakati katika ngazi
zote za shirika,” alisema Kamishna Meng’ataki.
Semina hii elekezi, iliongozwa na wataalamu kutoka Wizara ya
Fedha wakiongozwa na Msaidizi Mkaguzi Mkuu wa ndani Bw. Abrahamu Elisamia
Msechu, ambaye aliendesha mafunzo katika kuimarisha utekelezaji wa Usimamizi wa
Viatarishi, huku Dkt. Bernard Mnzava kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM)
akitoa mafunzo ya kina kuhusu mbinu bora za usimamizi wa viatarishi ili kufikia
malengo.
Sambamba na hayo, mafunzo ya vitendo yalifanyika kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Viatarishi wa TANAPA, Risk Information Management System (RIMS), ambapo Maafisa wa kutoka kitengo cha TEHAMA walionyesha namna bora ya matumizi ya mfumo huo katika usimamizi wa viatarishi.





0 Maoni